Umoja wa Mataifa (UN) umeahidi kuendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali za Tanzania za kuiletea maendeleo, ikiwemo kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa UN, Amina Mohammed alipofika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika mazungumzo hayo, Amina amewasilisha salamu kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na kumpongeza na amempongeza kwa jitihada anazochukua dhidi ya janga la UVIKO 19.
Amemwahidi kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kuhakikisha kuwepo na usawa wa upatikanaji wa chanjo na wanaendelea na majadiliano na taasisi za kifedha kuona ni jinsi gani zinasadia nchi zinazoendelea kukabiliana na ugonjwa huo.
Vilevile, ameahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.