Unaweza ukashinda kura za maoni bado nikakukata: Rais Magufuli

0
45

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufulia amewataka viongozi aliowateua kuridhika na kuzitumikia nafasi walizonazo kwa sasa, badala ya kuanza kuhangaika na nyingine ambazo hawana uhakika wa kuzipata.

Rais ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibu ambao ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na Mkuu wa Wilaya ya Monduli.

Akimtolea mfano Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro, Rais Magufuli amesema atamshangaa kiongozi huyo endapo ataamua kwenda Bunda kugombea ubunge ili aje kuteuliwa kuwa waziri wakati yeye (Rais) alimteua kuliongoza jeshi la polisi.

“… nitamshangaa sana kama ataenda kugombea ubunge Bunda, akitegemea nitamteua kuwa waziri. Kwanza hana uhakika kama atashinda kura za maoni, inawezekana akashinda, bado nikamfuta, na itatokana na siku hiyo nimeamkaje,” amesema Rais.

Amesisitiza kuwa mtu kushinda kura za maoni sio tiketi ya kugombea kwani Chama cha Mapinduzi (CCM) huko nyuma kimewahi kuwakata watu watatu wa mwanzo na kumchagua mshindi wa nne.

“CCM tumewahi kuteua mtu ambaye hakuwa hata wa kwanza nafikiri ni [Damas] Ndumbaro, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje alikuwa wanne kwa washindi kwenye kura za maoni. Wa kwanza tukamtia cross, wa pili tukamtia cross, wa tatu tukamtia cross, tukamchagua wanne, sasa watu hawaelewi historia,” amesema Rais.

Rais amewataka viongozi kuridhika kwa sababu mtu hawezi kuwa na kila kitu, lakini akasema mtu akiona kwamba anaweza kugombea na akashinda, aende kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.

“Mimi nafikiri saa nyingine ni kuridhika, kila mahali unaweza kufanya maajabu katika nafasi yako, otherwise [vinginevyo] haiwezi ukawa na kila kitu,” amesema Rais Magufuli akitilia mkazo.

Send this to a friend