Uongozi wa Rais Samia waleta mafanikio katika sekta ya benki nchini

0
56

Sera bora za uchumi tangu Rais Samia Suluhu Hassan achukue madaraka zimeleta mafanikio makubwa kwenye sekta ya benki nchini Tanzania ambapo benki za biashara zimevunja rekodi kwa mapato na faida mwaka jana, huku uchumi ukionekana kukua kwa kasi.

Tangu Rais Samia kuingia madarakani mwezi Machi 2021 yamekuwepo mafanikio ambayo yamechochea maendeleo katika sekta ya fedha nchini na kuleta manufaa kwa wananchi ikiwemo kufungua matawi mengi zaidi nchini, na hivyo kutoa fursa za ajira kwa Watanzania pamoja na ongezeko la idadi kubwa ya mikopo inayotolewa kwa sekta binafsi, hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Taarifa za robo ya nne ya mwaka (Oktoba-Desemba 2023) za mabenki zinaonesha kuwa Benki za CRDB na NMB zimeendelea kuongoza katika sekta ya fedha ambapo Benki ya NMB imeweka rekodi ya faida ghafi ya Shilingi bilioni 775 kwenye kipindi cha mwaka mmoja kinachoishia Desemba 31,2023 pamoja na kufungua matawi mapya manne na kuajiri wafanyakazi wapya 98.

Kwa upande wa CRDB, benki hiyo ilipata faida ghafi ya Shilingi bilioni 599 mwaka jana. Pia, imeongeza jumla ya mali na amana za wateja, na kufanikiwa kuongeza kiasi cha mikopo inayotolewa.

Kutokana na uchumi wa Tanzania kukuwa kwa kasi chini ya Rais Samia, Benki ya CRDB mwaka jana iliongeza kiasi cha mikopo inayotoa hadi kufikia TZS trilioni 8.8 na pia umeiwezesha CRDB kufungua matawi 10 mapya nchini mwaka jana na kuajiri wafanyakazi wapya 232.

Hali hii inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi na gawio kutoka kwa benki ambazo serikali inamiliki hisa.

Kwa ujumla, mazingira mazuri ya uchumi chini ya uongozi wa Rais Samia yanatarajiwa kuleta mafanikio zaidi kwa sekta ya benki na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini Tanzania.