Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kuwekeza shilingi bilioni 2.7 ili kuanzisha huduma ya upandikizaji uloto na kupunguza gharama za matibabu hayo kwa wananchi.
Amesema hayo wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma mara baada ya kuzindua huduma za kibingwa za upandikizaji wa uloto hasa kwa watu wenye Selimundu (Sickle Cell).
“Upandikizaji uloto unatoa nafuu kubwa sana kwa wagonjwa wa selimundu kwani huwapunguzia kwa kiasi kikubwa maumivu na maambukizi ya mara kwa mara, na wakati mwingine huwa sababu ya kupona kabisa kwa ugonjwa huu wa kudumu. Kutokana na nafuu hiyo, mgonjwa huweza kuishi maisha yenye ubora na kushiriki vema katika shughuli mbalimbali ikiwemo masomo,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa inakuwa hospitali ya pili baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuzindua huduma hiyo ya upandikizaji wa uloto, na hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa hospitali chache zinazotoa huduma hiyo katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Ameongeza kuwa uzinduzi wa huduma hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ni ushahidi tosha wa namna ambavyo Tanzania inapiga hatua kuboresha huduma za afya nchini.