Ureno kuwekeza kwenye bandari ya uvuvi Tanzania

0
13

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Ureno, Marcelo Rebelo de Sousa, Ikulu mjini Lisbon, nchini Ureno.

Viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Ureno hususani katika sekta ya uchumi wa buluu kwa kutumia rasilimali za bahari.

Aidha, Dkt. Mpango amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na ukanda mrefu wa pwani wa takribani kilomita 1,450 na ukanda wa kiuchumi wa kipekee unaofikia kilomita za mraba 223,000 hivyo ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili utakua na manufaa zaidi.

Kwa upande wake Rais Marcelo amesema Ureno ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kujenga bandari ya uvuvi itakayosaidia Tanzania kunufaika zaidi kupitia rasilimali za bahari na kupiga hatua za kimaendelea katika kuimarisha uchumi wa buluu, pamoja na kukuza sekta ya biashara na uwekezaji.

Makamu wa Rais yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake wenye lengo la kuhamasisha juhudi za mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa lengo la 14 la maendeleo endelevu.

Send this to a friend