Urusi kujengea kinu cha nyuklia nchini Burkina Faso

0
52

Viongozi wa kijeshi wa Burkina Faso wamesaini makubaliano na nchi ya Urusi ya kujenga kinu cha nyuklia ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini humo.

Makubaliano hayo na Urusi ni matokeo ya mazungumzo kati ya kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore, na Rais wa Urusi Vladimir Putin mwezi Julai wakati wa mkutano wa Urusi-Afrika huko Moscow.

“Kuna hitaji kubwa sana la nishati, hili ni jambo muhimu kwetu kwa sababu tunahitaji, ikiwezekana kujenga kituo cha kuzalisha umeme cha nyuklia nchini Burkina Faso,” alinukuliwa akisema wakati huo.

Aliongeza kuwa “Nafasi yetu ni ya kimkakati kwa sababu tuko katikati ya Afrika Magharibi na tunakabiliwa na upungufu wa nishati katika eneo hili.”

Burkina Faso ni moja ya nchi zenye upungufu wa nishati ya umeme ulimwenguni, na asilimia 21 ya watu pekee ndio waliounganishwa na nishati ya umeme, na kwa mujibu wa shirika la maendeleo la Marekani, Burkina Faso pia ni moja ya nchi zenye gharama kubwa zaidi za umeme barani Afrika.

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imegeukia Urusi kwa msaada wa kiuchumi na kijeshi tangu ilipochukua madaraka mwaka jana.

Send this to a friend