Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Rais wa China, Xi Jinping wametia saini ushirikiano mpya wa kimkakati kati ya nchi zao na kutoa wito wa suluhisho la kidiplomasia kwa vita vya Moscow dhidi ya Ukraine, japokuwa Putin amesema haoni dalili ya utayari kutoka kwa serikali ya Kyiv na washirika wake wa Magharibi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema Beijing na Moscow zinaamini kwamba Mkataba wa Umoja wa Mataifa lazima uzingatiwe na sheria ya kimataifa lazima iheshimiwe, lakini haikudai kwamba Urusi iondoe wanajeshi wake kutoka Ukraine au kuheshimu mipaka ya Ukraine inayotambuliwa kimataifa.
Rais wa Marekani aipongeza ICC kwa kutaka Rais Putin akamatwe
Lakini Ukraine imeisisitiza Urusi kujiondoa katika ardhi yake kama sharti la mazungumzo yoyote japokuwa hakuna dalili kwamba Urusi iko tayari kufanya hivyo.
Putin ameita mazungumzo yake na Xi kuwa ya wazi na ya kirafiki na yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wao wa bila kikomo uliokubaliwa mapema 2022, wiki tatu kabla ya Urusi kuivamia Ukraine.
Putin amesema, “Tunaamini kwamba vipengele vingi vya mpango wa amani uliotolewa na China vinaendana na mitazamo ya Urusi na vinaweza kuchukuliwa kama msingi wa suluhu ya amani wanapokuwa tayari kwa hilo katika nchi za Magharibi na Kyiv. Hadi sasa, hatuoni utayari kama huo kutoka kwa upande wao.”