Rais Samia Suluhu anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini Brazil ambapo atashiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la G20 utakaofanyika Novemba 18-19 mwaka huu jijini Rio de Janeiro.
Rais Samia amealikwa na Rais wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva na Mwenyekiti wa G20 kushiriki jukwaa hilo lenye lengo la kukuza ushirikiano wa kimataifa kwenye masuala ya kiuchumi ikiwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuhudhuria mkutano huo.
Mwaliko huo unatokana na heshima pamoja na ushawishi mkubwa ambao Rais Samia amejijengea kwenye majukwaa ya kimataifa.
Aidha, katika mkutano huo, Rais Samia anatarajia kushiriki mijadala inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa na umasikini, kuchochea maendeleo endelevu na matumizi ya nishati mbadala.
Rais Samia anatarajia kutumia jukwaa hilo linalokutanisha nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha usalama wa chakula, kupunguza umasikini, kujenga maendeleo endelevu na kutafuta fursa za ushirikiano zitakazowaletea ustawi Watanzania kupitia sekta za uzalishaji.
Akiwa nchini humo, Rais Samia atafanya mikutano ya pembezoni na taasisi kubwa za kifedha duniani pamoja na kuzungumza na Wakuu wa Nchi na Serikali na baadhi ya nchi wanachama wa G20 akiwemo mwenyeji wake Brazil, lengo likiwa ni kukuza na kuimarisha mahusiano hususan ni kwenye sekta ya viwanda, biashara, kilimo, nishati, utalii pamoja na kutafuta fursa mbalimbali za ushirikiano na uwekezaji.
Ushiriki wa Rais Samia kwenye mkutano huo, unalenga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuchangia ipasavyo mijadala muhimu ya kimataifa kuhusu maendeleo duniani na kunadi sera za uchumi za kimataifa zitakazochochea maendeleo na ustawi zaidi nchini Tanzania na barani Afrika.