Uswisi yaipa Tanzania msaada wa bilioni 39 kuboresha sekta ya afya

0
38

Tanzania imepokea msaada wa shilingi bilioni 39.59 kutoka serikali ya Uswisi unaolenga kusaidia jitihada za Tanzania kufikia malengo ya kusaidia sekta ya afya kwa wote na kupunguza malaria nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James ameeleza kuwa, Tanzania imesaini mikataba miwili ambapo mkataba wa kwanza ni msaada wa shilingi bilioni 24.51 ambazo zimetolewa ili kugharamia mradi wa uboreshaji wa afya na uimarishaji wa mfumo wa afya (HPSS), na mkataba wa pili ni wa msaada shilingi bilioni 15.08 zimezotolewa kwa ajili ya kugharamia programu ya kutokomeza malaria nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chassot amesema Serikali ya Tanzania na Uswisi wana uhusiano mzuri kwa muda mrefu sasa na wametoa msaada huo ili kuisaidia Tanzania kujiimarisha katika Sekta ya Afya ikiwemo kupambana na kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini Tanzania.

“Mpango mpya wa malaria ambao tumeusaini leo utaenda kumaliza malaria nchini Tanzania kwa faida ya watu wanaoishi hapa,” amesema Didier Chassot.

Naye mkurugenzi wa kinga Wizara ya Afya Dkt. Leornard Sudi amesema Wizara ya Afya itaenda kutumia fedha hizo vizuri kwa kuimarisha mifumo ya afya na takwimu kwa ujumla ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na malaria ambapo mpaka sasa vimepungua kwa zaidi ya asilimia 67.

“Kwa msaada huu ambao tumeupata wa Bilioni 39.59 tutaendeleza kuimarisha mifumo ya takwimu, sisi tunaelewa kwamba takwimu ndio zitaonesha namna gani tunavyozidi kuendelea,” amesema Dkt. Sudi.

Send this to a friend