Utafiti: 5.8% wanaotumia dawa za VVU wana tatizo la usugu

0
42

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) umeonesha asilimia 5.8 ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) na kutumia dawa wanakabiliwa na tatizo la usugu.

Akizungumza Mtafiti Mwandamizi Kitengo cha Maikrobaiolojia na Kinga MUHAS, Dkt, Doreen Kamori amesema utafiti huo ulifanyika mwaka 2020 katika mikoa 22 Tanzania Bara ikiwemo Mbeya, Songea, Iringa na Njombe.

Amesema sababu zinazochangia tatizo hilo ni pamoja na kuingizwa nchini dawa ambazo zinachangia usugu na watu kutotumia dawa ipasavyo huku akitoa ushauri kwa serikali kuweka miongozo na kufanya utafiti kufahamu wingi wa VVU kwa wagonjwa pindi wanapofikiria kubadilisha dawa na kuingiza nchini.

“Ni vyema kuweka miongozo na kujiandaa vizuri kumudu tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za kupunguza makali ya VVU au kudhibiti kabla ya dawa hizo kuleta madhara,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Prof. Said Aboud amesema tatizo hilo linazidi kuongezeka kwa sababu WAVIU wanaendelea kutumia dawa maisha yao yote, hivyo ni muhimu kuweka mikakati ikiwemo kufuata maelekezo ya wataalamu na mwongozo unaotakiwa wakati wa kutumia dawa hizo.

Aidha, Kaimu Makamu Mkuu MUHAS, Prof. Emmanuel Balandya amesema asilimia 4.5 ya watu wazima sawa na watu 1,548,000 wanaishi na VVU ambapo kati ya hao wanaotumia dawa, 87asilimia tano tayari wana usugu wa vimelea dhidi ya dawa (UVIDA).

Chanzo: Nipashe