Je! Huwa unaoga kila siku? Kama jibu lako ni ndiyo, basi jua kuwa hauko peke yako.
Katika maeneo mengi duniani watu huoga kila siku, lakini nchini China chapisho la Harvard Healthy linaeleza kuwa nusu ya watu huoga mara mbili tu kwa wiki.
Lakini umewahi kujiuliza kwanini watu wengi huoga kila siku? Pengine jibu lako ni sababu za kiafya. Kwa mujibu wa Harvard, kuoga kila siku kwa watu wengi ni utamaduni au utaratibu wa kijamii zaidi kuliko suala la kiafya. Na hii huenda ndiyo sababu suala la watu kuoga hutofautiana kutoka nchi moja na nyingine.
Mbali na suala la kiafya, baadhi ya watu wamesema huoga kila siku ili kutoa harufu mbaya mwilini, kuwasaidia kuondoa usingizi, ni sehemu ya wao kufanya mazoezi. Lakini ni wazi pia kuwa kuoga kila siku kunaweza kuwa njia ya makampuni ya bidhaa za kusafisha mwili kuendeleza biashara zao.
Linapokuja suala la afya, haijathibitishwa kuwa kuoga kila siku kuna mchango kiafya. Tena inaelezwa kuwa kuoga kila siku kunaweza kuwa na matokeo hasi kama vile kuifanya ngozi kuwa kavu kwa kuisugua hasa kwa maji moto.
Kwa kawaida, ngozi yenye afya huwa na kiasi fulani cha mafuta, uwiano mzuri wa bakteria na viumbe vingine vidogo (microorganisms). Unapooga unaondoa hivi vyote na hivyo ngozi inaweza kuwa kavu na kupauka. Ngozi kavua na yenye mpasuko inaweza kuruhusu bakteria wenye madhara (allergens) kupenya na kusababisha athari za ngozi.
Chapisho la Harvard linaeleza pia sabuni za kuoga za kuua bakteria (antibacterial) zinaua bakteria wanaotakiwa kwenye ngozi. Hii huathiri uwiano wa viumbe hao kwenye ngozi, na huweza kupelekea uwepo wa viumbe wasio rafiki ambapo hawasikii dawa.
Mfumo kinga wa ngozi unahitaji kichochea kutoka kwa bakteria, uchafu na vitu vingine vya kwenye mazingira ili kuweza kujitengemezea kinga. Hii ni moja ya sababu ya wataalamu wa ngozi kushauri watoto wasiogeshwe kila siku kwani kufanya hivyo kunaweza kuipunguzi ngozi uwezo wa kujitengenezea kinga yake.
Aidha, sababu nyingine ya kukufanya usioge kila siku inaweza kuwa maji unayotumia. Maji ambayo hutumiwa kusafisha mwili yanaweza kuwa na chumvi, kemikali mbalimbali au madini (heavy metals, chlorine, fluoride) na dawa za kuuwa wadudu. Vyote hivi vinaweza kuwa na madhara kwenye ngozi.
Hata hivyo, licha ya kuwa hakuna kiwango kinachokubalika kwa wote kuhusu suala la kuoga, wataalamu wanashauri kuwa kuoga mara kadhaa kwa wiki kunafaa kwa watu wengi. Lakini unaweza kuoga mara kwa mara ikiwa umetokwa jasho, uchafu kama vile vumbi, moshi, au sababu nyingine ya kukufanya uoge.
Kama sababu ya kukufanya uoge kila siku ilikuwa ni ya kiafya, basi unaweza kupunguza idadi hiyo.