Utafiti: Kuzuiwa kwa USAID kunaweza kusababisha vifo zaidi ya milioni 14 ifikapo 2030

0
155

Utafiti umebini kuwa kupunguzwa kwa kiasi kikubwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) na uwezekano wa kuvunjwa kwa shirika hilo kunaweza kusababisha vifo vya ziada zaidi ya milioni 14 ifikapo mwaka 2030, kwa mujibu wa jarida la tiba la The Lancet.

Tangu kuingia madarakani Januari, utawala wa Rais Donald Trump ulianza kupunguza ufadhili kwa USAID na miradi yake duniani kote, kwa madai kuwa ni sehemu ya mpango mpana wa kuondoa matumizi yasiyo ya lazima.

Hata hivyo, wataalamu wa haki za binadamu wameonya dhidi ya hatua hiyo, wakisema kuwa ufadhili wa USAID umekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha afya duniani, hasa katika nchi za kipato cha chini na cha kati, hususan barani Afrika.

Hata hivyo, utafiti huo umebaini kuwa kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, miradi ya USAID imezuia zaidi ya vifo milioni 91 duniani kote, wakiwemo watoto milioni 30.

Umetahadharisha kuwa iwapo ufadhili utaendelea kupunguzwa kwa kiwango kikubwa, na ikitokea USAID ikavunjwa kabisa, basi huenda kukatokea vifo vya zaidi ya watu milioni 14 ifikapo 2030, wakiwemo watoto milioni 4.5 walio chini ya umri wa miaka mitano.

Marekani ndio mfadhili mkubwa zaidi wa misaada ya kibinadamu duniani, ikitoa asilimia 38 ya misaada yote ya kimataifa iliyoripotiwa kwa Umoja wa Mataifa.

Send this to a friend