Utafiti: Masalia ya ARV yabainika kwenye nyama ya kuku na nguruwe

0
14

Utafiti uliofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) mwaka 2024, na kuchapishwa Machi 28, 2025 katika jarida la kimataifa la Springeropen, umegundua uwepo wa masalia ya dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARV) kwenye nyama na damu za kuku wa kisasa (broiler) na nguruwe nchini Tanzania.

Utafiti huo uliofanyika katika wilaya tisa, ukihusisha sampuli 196 za damu na nyama, matokeo yake yameonesha kuwa sampuli 131, sawa na asilimia 66.8, zilikuwa na masalia ya dawa ya ARV aina ya Lamivudine. Masalia hayo yamepatikana kwa kiwango cha 7.58 mg/kg kwenye nyama na damu, na kiwango kidogo cha 0.001 mg/kg kwenye chakula cha kuku wa kisasa. ​

Watafiti wanaeleza kuwa wakulima wanaoishi na VVU huenda wanatumia ARV wanazopewa kuwapa wanyama, jambo ambalo linaweza kusababisha kutofuata matumizi ya dawa ipasavyo na kuibuka kwa usugu wa dawa.

Mbali na matatizo ya moja kwa moja ya afya ya binadamu na wanyama, mabaki hayo kwenye chakula cha wanyama na kinyesi,yameelezwa kuwa yanaweza kusababisha uchafuzi wa mazingira na kuleta madhara kadhaa. ​

Utafiti: Mbege inapunguza uvimbe na kuboresha kinga ya mwili

Aidha ripoti hiyo imeshauri kutolewa kwa elimu kwenye jamii na wafugaji kuhusu hatari za matumizi ya ARV kwa wanyama pamoja na Serikali kuandaa miongozo madhubuti na sheria kali kuhusu matumizi ya dawa ARV ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa kina juu ya matumizi yake.

Pia imeshauri ukaguzi wa mara kwa mara kwenye masoko ya bidhaa za wanyama kuhakikisha hakuna mabaki ya dawa hizio na kufanya utafiti kubaini chanzo cha matumizi hayo kwa mifugo.

Baadhi ya wafugaji au wasambazaji wa chakula cha kuku wameripotiwa katika baadhi ya tafiti kutumia dawa za binadamu kama ARVs kwa lengo la kuongeza ukuaji wa kuku haraka, kupunguza maambukizi au kuongeza kinga.

 

 

 

Send this to a friend