Utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonesha watu wanaofanya mazoezi mepesi na yale ya kuimarisha misuli wanaweza kuishi maisha marefu zaidi.
Watafiti kutoka nchini Marekani wamegundua kuwa shughuli zinazoimarisha misuli kama vile kunyanyua vitu vizito, zinapaswa kuwa sehemu ya mazoezi ya kila wiki pamoja na mazoezi mepesi (aerobics) yanayojumuisha kukimbia na kuogelea.
Watafiti wameshauri si lazima kwenda sehemu za mazoezi (gym) badala yake watu wanaweza kutumia mifuko mizito, kufanya kazi ngumu au kutembea kwa haraka. Pia kulima shambani ni muhimu kwa watu waliozidi umri wa miaka 65.
Watu wazima walio na umri wa zaidi ya miaka 65 wanashauriwa kufanya mazoezi ya viungo kila siku. Wanahitajika kufanya shughuli za kuimarisha nguvu na mazoezi mepesi angalau mara mbili kwa wiki.