Utafiti: Mbege inapunguza uvimbe na kuboresha kinga ya mwili

0
9

Utafiti mpya uliofanyika nchini Tanzania na kuchapishwa na jarida kubwa la Nature Medicine la nchini Uingereza, umebaini kuwa lishe ya asili ya Kiafrika ina faida kubwa kwa afya ya binadamu ikilinganishwa na lishe ya Kimagharibi.

Pia imebaini kuwa kubadili aina ya chakula hata kwa muda mfupi kunaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye kinga ya mwili na hali ya kiafya kwa ujumla.

Utafiti huo uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha KCMC na Taasisi ya Utafiti ya KCRI nchini ulihusisha wanaume 77 wenye afya njema kutoka maeneo ya mijini na vijijini. Washiriki waligawanywa katika makundi ambapo baadhi walibadili lishe yao kutoka ya Kiafrika kwenda ya Kimagharibi, wengine walibadili kutoka ya Kimagharibi kwenda ya Kiafrika, na kundi lingine lilikuwa likinywa kinywaji cha jadi cha ndizi kilichochachushwa kiitwacho mbege.

Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa wale waliobadili lishe kwenda ya Kimagharibi walionesha kuongezeka kwa protini za uvimbe kwenye damu, kushuka kwa uwezo wa kinga ya mwili na kuanza kwa dalili za magonjwa kama kisukari na magonjwa ya moyo. Kinyume chake, waliorejea kwenye lishe ya Kiafrika au waliotumia mbege walionyesha kupungua kwa viashiria vya uvimbe, na hali yao ya kinga ya mwili kuboreka.

Daktari wa kinga ya mwili kutoka Chuo Kikuu cha KCMC, Dkt. Godfrey Temba, amesema kuwa huu ndio utafiti wa kwanza kuchunguza kwa kina athari za lishe ya Kiafrika.

“Watu wengi wanahamia kwenye miji na kuacha vyakula vyao vya asili, hali inayochangia kuongezeka kwa magonjwa ya kisasa. Lakini utafiti huu umeonesha wazi kuwa hata mabadiliko ya muda mfupi kwenye lishe yanaweza kusaidia mwili kupambana na uvimbe na kuimarisha afya,” amesema Dkt. Temba.

Dkt. Temba ameongeza kuwa lishe ya Kiafrika yenye mboga nyingi, matunda, maharage, nafaka asilia na vyakula vya kuchachushwa inaweza kuwa suluhisho la kiafya kwa bara la Afrika na duniani kwa ujumla, hasa wakati huu ambapo vyakula vilivyosindikwa vinaongezeka kwa kasi.

Kwa mujibu wa watafiti, baadhi ya madhara au faida za mabadiliko ya lishe zilibaki kuonekana hata wiki nne baada ya utafiti, jambo linaloonesha kuwa mlo wa mtu una athari ya muda mrefu kwenye afya.