
Utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa ndoa huongeza mara tatu zaidi hatari ya unene kwa wanaume, lakini haina athari sawa kwa wanawake.
Utafiti huo, uliofanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Moyo nchini Poland na kuwasilishwa kwenye Kongamano la Ulaya kuhusu Unene huko Málaga, Uhispania, umebaini kuwa ndoa inaongeza uwezekano wa kuwa na uzito mkubwa kwa asilimia 62 kwa wanaume na asilimia 39 kwa wanawake.
Matokeo hayo yanaenda sambamba na utafiti wa awali uliofanywa nchini China mwaka 2024, ambao ulibaini kuwa uzito wa wanaume huongezeka ndani ya miaka mitano ya kwanza ya ndoa kutokana na ongezeko la ulaji wa kalori na kupungua kwa shughuli za mwili.
Utafiti wa awali uliofanywa na Chuo Kikuu cha Bath uligundua kwamba, kwa wastani, wanaume waliooa walikuwa na uzito wa kilo 1.4 zaidi kuliko wenzao wasiooa.
Aidha, utafiti uligundua kwamba umri pia ulikuwa ni kiashiria muhimu cha ongezeko la uzito, ambapo kadiri umri unapoongezeka kila mwaka, huongeza hatari ya kuwa na uzito mkubwa kwa asilimia 3 kwa wanaume na asilimia 4 kwa wanawake, na hatari ya unene kupita kiasi huongezeka kwa asilimia 4 kwa wanaume na asilimia 6 kwa wanawake.
Hata hivyo, baadhi ya sababu zilionekana kuwaathiri wanawake pekee. Utafiti umeonyesha kwamba, kuwa na msongo wa mawazo huongeza mara mbili hatari ya wanawake kuwa na unene kupita kiasi, huku ukosefu wa uelewa wa masuala ya afya ukiiongeza kwa asilimia 43. Pia, wanawake wanaoishi katika jamii ndogo walionekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na unene kupita kiasi, tofauti na wanaume ambao hawakuathirika kwa viashiria hivyo.