Utafiti: Pombe zinasababisha mihemko ya kutaka kujamiiana

0
43

 

Licha ya Tanzania kuwa na Sheria ya Vileo na sheria nyingine ambatanishi, lakini matumizi holela ya pombe zenye asilimia kubwa ya kilevi yamekithiri mitaani na kusababisha madhara makubwa kwa jamii hasa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

Hayo yameelezwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge na Masuala ya UKIMWI, na kueleza kwamba licha ya jitihada za serikali na wadau wengine kupiga marufuku matumizi ya vileo vikali, bado vimeendelea kutumika mitaani.

“Hivi sasa imebainika kuwa vijana watumiaji wa pombe hizo wamegeukia kwenye chupa ndogo za plastiki zinazouzwa kwa bei nafuu,” imeeleza kamati na kwamba pombe hizo zina kiwango kikubwa cha kileo.

Kamati imetaja baadhi ya madhara ya pombe kali kuwa ni kubadilika kwa tabia, kuongezeka kwa ajali za barabarani, kuathirika kwa ini na figo na mihemuko kwa vijana kuwa na hamu ya kujamiiana.

Aidha, imeelezwa kwamba inahisiwa pombe hizo huwekewa madawa ya kulevya au dawa za kuongeza nguvu za kiume, na pia huchochea kasi ya maambukizi ya VVU kwa sababu ya kutotumia kondomu wakati wa kujamiiana kutokana na ulevi.

Kamati imeishauri Serikali kuchukua hatua za haraka za kupiga marufuku utengenezaji wa pombe zenye kilevi kikubwa ambazo zinawekwa kwenye chupa ndogo za plastiki. Kiwango cha chini kiwe miligramu 300 ili kupunguza matumizi mabaya ya pombe hizi ambapo zinauzwa hata sehemu za washona viatu na maeneo yasiyo rasmi.

Send this to a friend