Utafiti wa Wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) umebaini watu wanaotunza wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs), wana uwezekano wa kukumbwa na maradhi hayo.
Magonjwa hayo yametajwa kuwa ni yale ambayo hayaambukizi moja kwa moja kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine, ambayo ni kiharusi, magonjwa ya moyo, saratani, kisukari, magonjwa sugu ya figo na mengineyo.
Utafiti huo umeonesha hadi asilimia 96 ya watu wanaotoa huduma kwa wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza, walikuwa na angalau kisababishi kimoja cha kuwa katika hatari ya kupata maradhi hayo.
Vihatarishi hivyo ni pamoja na unywaji pombe, ulaji usiofaa, matumizi ya tumbaku, kutofanya mazoezi ya mwili, na sababu hatari za kibaolojia ikiwemo magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu pamoja na uzito wa ziada wa mwili.
Wanaume Katavi: Wanawake wakipata pesa wanatunyanyasa na kutunyima tendo la ndoa
Aidha, mratibu wa utafiti huo na mwanasayansi, Dkt. Pedro Pallangyo amesema pamoja na kushuhudia athari za magonjwa haya yasiyoambukiza kwa ndugu zao, watoa huduma bado huendelea kuishi kwenye tabia hatarishi zinazowaweka kwenye hatari ya kuugua.
“Sio kwamba hawana taarifa hizo, wanazo. Kwa sababu watoa huduma mara nyingi huwasindikiza ndugu na jamaa zao kwenda vituo vya afya, kwa hiyo wanapata taarifa na elimu kutoka kwa watoa huduma lakini bado shida iko pale pale. Taarifa zipo lakini utekelezaji katika kubadili mienendo ya maisha bado ni changamoto,” amesema Pallangyo.
Chanzo: Mwananchi