Utafiti: Wanasayansi wasema huenda corona inaambukizwa kwa kujamiiana

0
37

Mjadala mkubwa umeibuka tena duniani baada ya mtafiti kutoka nchini China kubaini uwepo wa virusi vya corona katika shahawa za mwanaume, hivyo kuibua mjadala juu ya uwezekano wa ugonjwa huo kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana.

Uchunguzi uliofanywa na daktari kutoka katika Hospitali ya Manispaa ya Shangqiu nchini China umehusisha wanaume 38 wenye maambukizi ya homa ya mapafu (COVID-19), ambapo sita kati yao, sawa na 16%, walikuwa na virusi hivyo kwenye shahawa.

Watafiti wameeleza kuwa, kutokana na tukio hilo kuwa la awali na lililohusisha watu wachache, uchunguzi zaidi unahitajika ili kujiridhisha kama Covid-19 inaweza kuambukizwa kwa kujamiiana.

“Endapo itathibitika kuwa virusi hivyo vinaweza kuambukizwa kwa kujamiiana, hilo litaweka ugumu sana katika kudhibiti maambukizi, hasa kutokana na ukweli kwamba virusi hivyo vimepatikana kwa watu ambao wameanza kupoka,” wamesema watafiti.

Utafiti mdogo uliofanyika mwezi Februari na Machi mwaka huu uliohusisha wagonjwa 12 wa COVID-19 nchini China ulionesha kuwa mbegu za kiume za wagonjwa hao hazikuwa na maambukizi.

Profesa Allan Pacey kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza amesema majibu ya sasa yasiwe hitimisho, na kwamba chunguzi zaidi unahitajika, ili kubaini pia kama virusi hivyo kwenye shahawa vinauwezo wa kusababisha madhara kwa mtu mwingine.

Send this to a friend