Utafiti: Wanywaji wengi wa pombe Dar wanauzito kupitia kiasi

0
12

Utafiti wa hivi karibuni umeonesha kwamba asilimia 67.2 ya wakazi wa Dar es Salaam wana uzito kupita kiasi huku wengi wao wakiwa ni wanywaji wa pombe wa mara kwa mara.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo amesema utafiti huo ulifanyika mwaka 2020 ukihusisha watu 6,691.

Serikali yashauri wananchi kuongeza ulaji wa nyama na mayai

Amesema utafiti huo mkubwa Zaidi kuwahi kufanyika nchini ulihusisha wanawake na wanaume wenye umri wa wastani wa miaka 43.1 ambapo asilimia 54.2 walikuwa ni wanaume hivyo wanawake walioneka kuwa na uzito uliokithiri zaidi ikilinganishwa na wanaume.

Amebainisha kwamba katika suala la ulaji, utafiti umeonesha watu wanaokula vyakula vya nje ya nyumbani wakinunua katika migahawa, wameonekana kuwa na uzito mkubwa ikilinganishwa na wale wanaokula nyumbani.

“Kikubwa ni kwamba wanakula si kwa sababu hawana nidhamu ya muda wa kula, wanakula muda wowote na wanaishia kula chakula ambacho si kizuri kiafya” ameeleza.

Aidha, Dk Pedro amesema waliangalia pia mwenendo wa ulaji wa mbogamboga na matunda kwa siku kulingana na mapedekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na kubaini wale waliokuwa na ulaji mdogo kuliko inavyopaswa walikuwa kwenye hatari ya kupata uzito uliokithiri pamoja na watu wenye shinikizo la juu la damu, wanywaji pombe na watu wasiozingatia unywaji wa maji nao pia wako katika hatari hiyo.