Utaratibu wa kufuata unapopoteza kitambulisho chako cha taifa nchini Tanzania
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetoa maelekezo kuhusu hatua za kufuata mtu anapopoteza kitambulisho chake ili aweze kupata kitambulisho kipya.
NIDA imelazimika kutoa maelezo hayo baada ya mtumiaji mmoja wa mtandao wa kijamii kuhoji kwanini utoaji wa pasi za kusafiria za kielektroniki unakulazimu kuwa na kitambulisho cha taifa. Mtu huyo alihoji itakuwaje kwa wale watakaokuwa wamepoteza vitambulisho vyao na wanahitaji pasi za kusafiria.
NIDA wameeleza kwamba, yeyote aliyepoteza kitambulisho chake atatakiwa kutoa taarifa polisi lakini pia atalipia TZS 20,000 ambayo ni gharama ya kuweza kutengenezewa kitambulisho kingine.
“Fika kwenye ofisi yetu ya usajili Wilaya unayoishi /uliyojisajili, utapatiwa fomu kwa ajili ya kupeleka polisi ili upatiwe Loss Report (taarifa ua upotevu), pamoja na fomu yenye namba ya akaunti kwa ajili ya kufanya malipo ya TZS 20,000/= gharama za kuzalisha kitambulisho kipya.”
Aidha, NIDA wamesema baada ya kupatiwa taarifa hiyo ya kupotea kwa kitambulisho, ataiwasilisha katika ofisi zao kwa ajili ya kuanza mchakato wa kupatiwa kitambulisho kipya.
“Baada ya kukamilisha malipo, utawasilisha hati ya malipo pamoja na loss report kwenye ofisi yetu ya usajili ili kuanza utaratibu wa kutengenezewa na kupatiwa kitambulisho kingine.”