Utata waibuka baada ya Zimbabwe kupata miss ‘mzungu’

0
38

Kurejea kwa Zimbabwe katika shindano la Miss Universe baada ya miaka 22 limezua utata mkubwa baada ya mwanamke ‘mweupe’ kutangazwa kuwa mshindi wa shindano hilo.

Brooke Bruk-Jackson (21) ambaye ni mwanamitindo anatarajia kuiwakilisha nchi hiyo kwenye shindano la kimataifa litakalofanyika El Salvador Desemba mwaka huu.

Baada ya ushindi wake, Bruk-Jackson alisema, “Najivunia kuwa Mzimbabwe. Hii ni ya kushangaza na ya kusisimua kwa wakati mmoja. Nimeshikwa na hisia. Nina hamu ya kutekeleza majukumu yangu kama malkia wa Zimbabwe mwaka huu huko El Salvador. Nimekuwa mwanamitindo kwa miaka kadhaa huko Cape Town na nimekuwa nikisafiri kote ulimwenguni, lakini hii ndiyo mara yangu ya kwanza kushiriki katika mashindano kama haya.”

Utafiti: Wasichana wengi walioachwa na wapenzi wao hupata ukichaa

Ushiriki wa mtu mweupe katika shindano hilo umekumbwa na utata kuhusu masuala ya rangi na utaifa. Zimbabwe ina historia ya mahusiano ya kikabila ambayo yamegawanyika kutokana na ukoloni na utawala wa zamani wa Rais Robert Mugabe. Watu weupe Zimbabwe ni chini ya asilimia moja ya idadi ya watu ambao ni zaidi ya milioni 15, kulingana na sensa ya mwaka 2022.

Akihojiwa kwenye kituo kimoja cha televisheni Bruk-Jackson amesisitiza umuhimu wa kutokuwa na ubaguzi wa rangi na tamaduni katika mashindano hayo ya urembo. Amesema, “moja ya mambo yangu makubwa ni kwamba haijalishi unatoka nchi gani, ikiwa unatoka nchi ya Afrika, unaweza kushiriki bila kujali rangi yako, tamaduni yako au historia yako. Hakuna mtu anayepaswa kukufafanua kwa rangi yako, jinsi unavyoonekana, au umbo la mwili wako.”

Send this to a friend