Makala za wasomaji: TUELEZENI MMEFIKIA WAPI

0
32

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema mpaka sasa hakuna utaratibu mpya uliotangazwa kuhusu mfumo upi hasa wenye tija utakaotumika kuwapa vijana mikopo ya asilimia 10 kutoka kwenye mapato ya halmashauri ambayo ilisitishwa na Serikali.

Akiandika mwenyekiti wa UVCCM, Mohammed Kawaida amesema vijana wameendelea kukosa fursa hiyo muhimu ya kupata mitaji ambayo ingeweza kuwasaidia kiuchumi na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

“Mpaka sasa Serikali kupitia wizara husika haijaeleza vijana na umma wa Watanzania hatua gani imefikia katika mchakato wa kuweka utaratibu mpya kama alivyoagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati mikopo hiyo ikisitishwa.

Tunatambua nia ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwainua vijana katika kila sekta. Tunaona kazi kubwa inayoendelea kufanywa kwenye kilimo, elimu na kuvutia wawekezaji ili kutengeneza ajira zaidi. Suala la mikopo kwa vijana ni sehemu ya juhudi za Mheshimiwa Rais kuhakikisha wanainuka kiuchumi, hivyo basi ukimya kuhusu jambo hili tena ambalo pia lina maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu unatutia mashaka kama vijana,” amesema.

Ameongeza kuwa uwezeshaji wa mikopo kwa vijana ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, hivyo ni jukumu la kila mtendaji serikalini kuhakikisha kwamba anatekeleza ilani ya chama katika kuwatumikia Watanzania wa makundi yote.

Send this to a friend