Ukarabati wa awamu ya kwanza unaoendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa mkoani Dar es Salaam umefikia asilimia 95 na asilimia tano zilizobaki zinatarajiwa kukamilika ndani ya siku tano kuanzia leo.
Akikagua ukarabati huo leo Oktoba 9, 2023, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amesema tayari vyumba vinne vya wachezaji, sehemu ya kuchezea, vyumba vya waamuzi, afya na eneo la video za marejeo (VAR) umekamilika.
“Tayari taa za kisasa 320 za mfumo wa LED zimefungwa na kuna huduma ya mtandao wa bure kabisa kwa ajili ya watazamaji wa mechi ambao tutauzindua kati ya tarehe 17 hadi 19 mwezi huu kabla ya mchezo wa ufunguzi wa African Football League kati ya timu ya Simba na Al Alhy ya nchini Misri tarehe 20, 2023,” amesema.
Ameongeza kuwa katika eneo la watu mashuhuri na sehemu ya wandishi wa habari kazi iliyobakia ni ndogo ambayo itamalizika ndani ya siku hizo tano akiongeza kuwa mfumo wa sauti uwanjani tayari umerekebishwa.
Dkt. Ndumbaro amesema mfumo wa matangazo kidijitali utafungwa hivi karibuni na kuanza kufanya kazi rasmi Oktoba 20, 2023 huku akisistiza kuwa baada ya mchezo huo, ukarabati mkubwa wa awamu ya pili utaendelea.