Uwanja wa Mkapa wafungwa hadi Oktoba 20

0
30

Uwanja wa Benjamin Mkapa umefungwa hadi Oktoba 20 kupisha ukarabati utakaoendana na miongozo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Akizungumza Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu wakati akipokea ugeni wa timu ya wataalam African Football League ili kuanza maandalizi ya ufunguzi rasmi wa mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Oktoba 20 mwaka huu, amesema mazungumzo yao yalijikita zaidi kuangalia ubora wa Uwanja na maeneo ambayo yatafanyiwa ukarabati.

“Kwa hivi sasa mpaka Oktoba 20, 2023 hakutakuwa na mechi nyingine itakayochezwa kwenye uwanja huu wa Benjamin Mkapa ili kupisha maandalizi kwa sababu miongoni mwa vitu watakavyofanya African Football League ni pamoja na kufumua eneo la kuchezea mpira kwa gharama zao na watalirejesha kwenye hali ambayo unachezeka mpira,” amesema.

Aidha, Katibu Mkuu amesema Wizara hiyo tayari imeshaingia mkataba na mkandarasi ambaye ni ni Beijing Construction Engineering Group Co., Ltd. (BCEG) ambapo ukarabati wa awali utajumuisha masuala mbalimbali ambayo CAF wanahitaji yafanyiwe kazi mapema.

Yakubu ameongeza kuwa timu za Tanzania ambazo zimefuzu kucheza mashindano yanayoandaliwa na CAF kwa michezo ya awali wameshauriwa kutumia uwanja wa Azam uliopo Chamazi ambao unakubalika kwenye viwango vya Shirikisho hilo kwa michezo ya awali.