Ikiwa ni siku mbili baada ya video ya wimbo ‘Ameyatimba (Remix)’ ya msanii Whozu ambaye ameshirikiana na Billnass pamoja na Mbosso kuachiwa, baadhi ya watazamaji wamelalamikia video hiyo wakidai imeenda kinyume na maadili ya Kitanzania.
Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii baadhi ya watu wameonesha kutopendezwa na maudhui yaliyoonekana katika video hiyo ambayo inaonesha vitendo ambavyo baadhi wamevitafsiri kuwa vinachochea unyanyasi wa kingono (ubakaji) huku wengine wakilitaka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuingilia kati.
Video hiyo inaanza ikimwonesha mwanamuziki Mboso akiwasihi wenzake walio nje ya chumba wamzuie msichana aliyeonekana akitoka chumbani akikimbia nje, kuashiria kuwa hataki kujamiiana na Mboso. Video inaendelea ikiwaonesha rafiki zake hao wakimrejesha msichana chumbani, huku Mboso akionekana kumlazimisha kujamiiana naye, na mashairi yafuatayo yakisikia;
“Mshike huyo hatoki mtu, Nimeupaka mkongo hatoki mtu
Mshike huyo hatoki mtu, Alinitia usongo hatoki mtu
Alinitia usongo hatoki mtu, Kashanipiga sana vizinga
Leo kajichanganya kayatimba, Kanipiga sana vizinga
Leo kajichanganya kayatimba, Oya alitaka kunichukulia poa
Kumbe mi mwenyewe ni mtoto… ”
Bayoko ambaye ni mmoja wa watumiaji wa mtandao wa X ameandika “Bado kwenye jamii yetu kuna shida kubwa sana ya uelewa juu ya consent na the fine line between consensual sex and rape. Wengi wameaminishwa kwamba kumhudumia mwanamke inakupa free pass to her private parts which ethically/legally/socially/spiritually is so so wrong,” huku Givenality Edward akiandika, “Huu wimbo wa “Ameyatimba” sidhani kama unapush jambo zuri. Unafanya ubakaji kuonekana kama jambo la sifa.”
Waziri aagiza kumbi za starehe, MCs, wasajiliwe kabla ya Novemba 30
Pamoja na hayo, baadhi ya watazamaji, akiwemo Ally Domoso, wameunga mkono maudhui hayo, akieleza kuwa “Mbosso hajahamasisha ubakaji isipokuwa kama kioo cha jamii anaonesha hali ilivyo kwa vijana wengi hususani linapokuja swala la ngono. Kwahiyo ni vyema kutazama uhalisia kuliko kumshutumu mbosso ambaye amefanya kazi nzuri ya maudhui,” huku Sheyoka akisema “Mbosso ameamua kuonesha hadharani jinsi akili nyingi za vijana wa Kitanzania zilipo…this is going to be a teachable moment for many.”
Swahili Times imezungumza na Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana kuhusu jambo hilo na amesema “kwa sasa BASATA ipo katika majadiliano kuhusu video hiyo na hivi karibuni itatoa kauli.”