Vifo vya Saratani kufikia milioni 1 mwaka 2030

0
27

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimy amebainisha kuwa takribani wagonjwa wapya wa Saratani 40,000 hugunduliwa kila mwaka na karibu jumla ya watu 27,000 wenye Saratani hufariki dunia nchini Tanzania.

Waziri Ummy amesema hayo leo kwenye uzinduzi wa jengo la huduma za Saratani lililopo Hospitali ya Aga Khan iliyozinguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ambapo kituo hicho kitatoa huduma kwa wagonjwa 100 kwa siku.

Amesema, sehemu kubwa ya wagonjwa wa Saratani hapa nchini wamebainika kuwa ni wanawake wenye Saratani ya mlango wa kizazi ambapo Saratani hii pekee inachangia 25% ikifuatiwa na Saratani ya matiti kwa 10% ambapo kwa pamoja Saratani hizi zinachangia zaidi ya 33% ya wagonjwa wote na kwa pamoja zinachangia karibu nusu ya vifo vyote vinavyotokana na Saratani hapa nchini.

“Vifo vitokanavyo na Saratani vitaongezeka ifikapo mwaka 2030 kama hatutachukua hatua za kushughulikia ukubwa wa tatizo hili la Saratani nchini ambapo inakadiriwa kufikia vifo milioni moja kwa mwaka 2030,” amesema Waziri Ummy.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia ametupatia bilioni 10 mwaka huu, tumesomesha madaktari bingwa na bozezi kwenye masuala ya Saratani zaidi ya 30 ambao tumewapeleka nje ya nchi ambao watakuja kusaidia kupunguza tatizo la Saratani nchini,” amesema Waziri Ummy.

Send this to a friend