Vifurushi vya Bima ya Afya kwa Wote vinavyopendekezwa na Serikali

0
42

Kiwango cha kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ni TZS 340,000 kwa kaya ya watu sita akiwemo mchangiaji, mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne kwa mwaka pindi sheria hiyo itakapojadiliwa na kupitishwa na bunge.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi na kuongeza kuwa kwa wale ambao hawana familia watachangia TZS 84,000 kwa mtu mmoja mmoja kwa mwaka ambayo ni sawa na wastani wa TZS 7,000 kwa mwezi.

Prof. Makubi amebainisha kuwa kwa wananchi watakaotambuliwa kutokuwa na uwezo wataendelea kupatiwa huduma kwa utaratibu utakaowekwa na Serikali kwa kila mtu kuwa na kadi yake ya Bima ya Afya.

“TASAF na mifumo ya maendeleo ya jamii ndio itakayofanya utambuzi kwa wananchi wasio na uwezo ili kuiwezesha Serikali kuweka utaratibu madhubuti wa kutoa huduma kwa wananchi wasio na uwezo kupata huduma pindi wanapohitaji,” amesema Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi ameweka wazi kuwa endapo sheria itapitishwa basi Wizara imejipanga kuanza mara moja utekelezaji wa sheria hii bila kikwazo ifikapo Julai 1, 2023 kwani suala hilo sio la ghafla.

Send this to a friend