Vigogo wa Shirika la Bima la Taifa wakabiliwa na mashitaka 365

0
26

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Samuel Kamanga na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka 365 yakiwemo ya kughushi na kutakatisha fedha.

Wakisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu, Evodia Kyaruzi na Wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Mwanga pamoja na Ipyana Mwakatobe wamesema watuhumiwa hao wanatuhumiwa kuhujumu uchumi kiasi cha shilingi bilioni 1.8 ambacho ni mali ya shirika la NIC.

Katika mashitaka hayo 365, yapo ya kughushi nyaraka mbalimbali, kutakatisha fedha, kuongoza genge la uhalifu, kuchepusha fedha, kuwasilisha nyaraka za uongo na kulisababishia hasara shirika hilo.

Washitakiwa wengine ni Tabu Kingu, Victor Mleleu, Peter Nzunda, Kenan Mpalanguro, Lusubilo Sambo na Mafworo Ngereji.

Kutokana na muda wa mahakama kuisha, washitakiwa hao wamesomewa mashitaka 101 pekee, huku mashtaka mengine wakitarajia kusomewa Jumatatu Juni 5, mwaka huu.

Send this to a friend