Vilabu vitatu ikiwemo Azam vyapigwa faini kwa vitendo vinavyoashiria ushirikina

0
31

Azam FC imetozwa faini ya TZS milioni moja kwa kosa la wachezaji wake na mmoja wa maafisa wake wa ufundi kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina ikiwemo kumwaga kimiminika kwenye lango na katikati ya uwanja katika mchezo namba 222 dhidi ya JKT Tanzania.

Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) baada ya kikao chake cha Juni 5, mwaka huu kilichokaa kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi.

Aidha TPLB imempiga faini ya shilingi milioni moja Kocha wa magolikipa wa Coastal Union, Mansuri Lawi kwa kosa la kujihusisha na vitendo vilivyoashiria imani za kishirikina katika mchezo namba 209 dhidi ya Geita Gold FC.

TPLB imesema wakati wachezaji wakipasha moto misuli kocha huyo alionekana akiwa ameshika chupa yenye kimiminika kisha kumwaga kimiminika hicho langoni.

Mbali na klabu hizo, TPLB imeitoza faini ya shililingi milioni moja Geita Gold kwa kosa la wachezaji wake kufanya vitendo vinavyoashiria ushirikina katika mechi dhidi ya Simba SC, ambapo imesema wakati wa kufanya mazoezi ya kupasha moto misuli, baadhi ya wachezaji hao walionekana wakiweka vitu chini ya mlingoti wa kibendera cha kona.

Pia Kamati imeipiga faini ya shilingi laki tano klabu ya Biashara United kwa kosa la mmoja wa viongozi wake kuonekana kiwanjani akiwa na kitu chenye ncha kali ambacho alikitumia katika moja ya matukio yanayoashiria imani za kishirikina.

Send this to a friend