
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu ya umoja na amani, kupinga chuki, migawanyiko na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga mshikamano waTaifa.
Ametoa wito huo leo Desemba 25, 2025 aliposhiriki ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri la Azani Front jijini Dar es Salaam.
“Manufaa ya amani ni makubwa; huleta maendeleo ya kiuchumi, huimarisha ustawi wa jamii, na huwezesha kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda amani na usalama wa nchi pamoja na kuwajenga Watanzania hususani vijana kuthamini dhana ya uzalendo kwa nchi yetu.
“Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha umoja, amani, mshikamano na utulivu katika ukanda wetu na barani Afrika. Amani hii imejengwa juu ya misingi imara ya maadili, haki, kuheshimiana, uvumilivu na uzalendo,” ameeleza.
Kadhalika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za elimu na dini katika kuimarisha malezi ya watoto na vijana kwa kuwajengea misingi imara ya maadili na kuwaongoza kutumia vyema fursa za elimu, teknolojia na utandawazi kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.







