Viongozi wa dini waifikisha kesi ya Mbowe mezani kwa Rais Samia

0
44

Viongozi wa dini wametumia mkutano wao na Rais Samia Suluhu kuomba mamlaka husika kutumia busara ili kuangalia namna ya kumaliza kesi inayomkabili kiongozi wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake.

Viongozi wametoa ombi hilo wakati wa mkutano wao na Rais Samia Suluhu uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam kuhusu maendeleo ya nchi.

Mambo mengine yaliyojadiliwa ni elimu ambapo viongozi hao wamependekeza kuwepo kwa mjadala mpana kuhusu mfumo mpya utakaokidhi mahitaji ya sasa. Wamesema kuna umuhimu mkubwa wa elimu itayozalisha jamii ya wahitimu walioandaliwa kujiajiri badala ya kuajiriwa peke yake.

Aidha, viongozi hao wameomba serikali itafakari uwezekano wa kufuta kodi ya mapato kwenye fedha zinazopatikana kama misaada ya hiari ya wanachama na wafadhili kwa ajili ya kuendesha huduma zisizo za kibiashara zikiwemo huduma za wajane na yatima.

Mapendekezo hayo yaliowasilishwa na Nelson Kisare, Askofu mkuu wa wa kanisa la Menonite, Tanzania kwa niaba ya viongozi hao wa dini pia yameelezea kuporomoka kwa maadili na ongezeko kubwa la vitendo vya uhalifu vya wizi, ujambazi, udhalilishaji, ubakaji, ukatili kwa wanawake na watoto na mauaji katika jamii, hali ambayo imeanza kutishia amani na usalama wa rai ana mali zao.

Viongozi hao wamempongeza Rais Samia kwa kuonyesha kuwa karibu na viongozi wa dini huku wakisihi kuwepo kwa vikao endelevu kati ya serikali na madhehebu ya dini kwa ajili ya tathmini na ufuatiliaji wa karibu.

Vile vile, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amepongezwa na viongozi hao wa dini kwa ujenzi wa mahusiano bora na nchi jirani na pia jumuiya ya kimataifa. Masuala mengine aliyopongezwa ni kujenga fursa za uongozi kwa wanawake na kuulinda Muungano.

Send this to a friend