Rais Samia Suluhu anatarajia kupokea ugeni mkubwa wa viongozi kutoka nchi tatu kwa mwezi Januari na Februari mwaka huu lengo likiwa ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na mataifa mengine.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje, January Makamba amesema kesho Januari 22, 2024, Rais Samia atampokea Mheshimiwa Liu Guozhong, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China anayekuja nchini kwa ziara ya siku tatu.
Katikati ya ujio wa kiongozi huyo wa China, Januari 23 ya mwezi huu Rais Tanzania itapata ugeni mwingine wa Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Valdes Mesa atakayekuwa nchini kwa siku tatu lengo likiwa ni kukuza uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Baadhi ya mambo atakayofanya mbali na kukutana na viongozi wakuu wa Tanzania na Zanzibar atatembelea kiwanda kinachozalisha dawa ya Biolarvicide cha Kibaha na kusalimiana wa Watanzania waliosoma Cuba.
Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Poland, Andrzej Duda anatarajiwa kuwa na ziara ya kikazi tarehe 8 na 9, Februari, 2024 katika hatua ya kuimarisha diplomasia ya Tanzania na Poland ambazo zina uhusiano mzuri katika miradi ya maendeleo ya miundombinu, uhifadhi wa wanyama pori, elimu, maji na usimamizi wa mazingira, utalii, biashara na uwekezaji bila kusahau ushirikiano wa mabunge.
Mbali na viongozi hao kuja Tanzania, Rais Samia amealikwa kufanya ziara za Kitaifa Indonesia, Vatican na Norway. Hii ni ishara kuwa Tanzania inazidi kufungua mipaka yake kimataifa na kuwa ina ushirikiano mzuri wa kidiplomasia na mataifa mengine.