Viongozi wamshukia Askofu Gwajima sakata la chanjo

0
36



Baadhi ya viongozi na wanasiasa nchi wameonesha kutokubaliana na kauli iliyotolewa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akiwataka wananchi kutokubali kuchanjwa dhidi ya UVIKO19, kwa madai kuwa chanjo si salama.

Gwajima ambaye pia ni mbunge wa Kawe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) alisema hilo Jumapili Julai 25, 2021 wakati akihubiri kanisani kwake mkoani Dar es Salaam.

Mbali na kuwasihi wananchi kutokubali kuchanjwa, Gwajima alisema daktari au kiongozi yeyote atakayehimiza watu wachanjwe, atakufa, kwani yeye (Gwajima) hazungumzi kama yeye, bali kama mtumishi kutoka mbinguni.

“Mimi namtaka daktari atakayeshadadia [chanjo], nitakula naye meza moja, utakufa daktari. Daktari atakayeshadadia bila kutuambia ukweli amefanya analysis [uchambuzi] ya chemical content [kemikali zilizotumika] ya chanjo ya corona na madhara yake leo na miaka 10 ijayo, utakufa, asema Bwana wa majeshi,” alisema Gwajima huku akishangiliwa na waumini wake.

Kauli hiyo imepingwa vikali na viongozi ambapo wameeleza kuwa ni sahihi kufanyika kwa mjadala juu ya usalama wa chanjo, lakini kusema serikali imeleta ili kudhuru watu wake, haikubaliki.

“Ni hatari kupotosha watu wanaotuamini kuhusu mambo ambayo hatuna utaalam nayo. Mjadala kuhusu usalama wa chanjo ni sahihi lakini kiapo kwamba Serikali imeileta kuwadhuru watu si sahihi,” amendika Mbunge wa Bumbuli, January Makamba kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kwa upande wake Mbunge wa Nzega Vijijini, Dkt. Hamis Kigwangalla amesema “tumerithi nchi yenye kuruhusu mijadala, ndiyo maana Askofu Gwajima anatumia haki yake ya kusema. Lakini ukiwa na maadili kidogo tu na ukajua nafasi yako kwenye jamii, utajitenga na uongo na kusimama na ukweli, kwa sasa utajua ukiwa una ushawishi basi utashawishi watu vibaya.”

Aidha, Askofu Dkt. Fredrick Shoo amewahimiza wananchi kuendelea kujikinga dhidi ya maambukizi ya corona na kuwaonya viongozi wa dini kutokuhusisha chanjo ya corona na masuala ya shetani kwani huko ni kumjaribu Mungu.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo ameandika “Tuchague sayansi,” akilenga kuwasihi wananchi kutosikiliza maneno ya wanasiasa, bali wafuate sayansi.

Mbali na viongozi hao, wananchi kupitia mitandao ya kijamii pia wameonesha kutokuunga mkono kauli ya Gwajima, huku baadhi wakitaka mamlaka husika kumchukulia hatua kwa kile walichodai kuwa anapotosha watu ambao wanamwamini.

Hii si mara ya kwanza kwa Askofu Gwajima kupinga chanjo hiyo, itakumbukwa Mei 2021 alizungumza bungeni na kuishauri Serikali kuwa makini na madhara yanayoweza kujitokeza kwa wananchi iwapo Taifa litaruhusu chanjo hiyo.

Aliziita chanjo hizo za mwendokasi kwa sababu zimepatikana ndani ya muda mfupi tofauti na utaratibu wa kupata chanjo, na hakuna utafiti wa kutosha uliofanyika juu ya madhara yake kwa binadamu hasa kwa miaka ijayo.

Haya hivyo, kumekuwepo na mitazamo mingi juu ya chanjo za corona na usalama wake, ni hii kwa kiasi kikubwa inaathiri uwezo wa wananchi kufanya maamuzi kama endapo wakubali kuchanjwa ama la.

Send this to a friend