Virusi vipya vya mafua vyabainika kwa nguruwe China

0
38

Wanasayansi wamebaini uwepo wa aina mpya ya virusi vinavyosababisha mafua (flu) nchini China ambavyo vinahofiwa kuwa huenda vikasababisha janga la dunia.

Wataalamu hao wamesema virus hivyo vilivyobainika karibuni vinapatikana kwa nguruwe, na imeelezwa kuwa kuna uwezekano vinaweza kuongezeka kwa haraka na kuhamia kwa binadamu.

Licha ya kuwa hadi sasa havijawa tishio, lakini imeelezwa kuwa kuna dalili zote kuwa vinaweza kuathiri binadamu, hivyo kuhitaji ufuatiliaji wa karibu.

Kutokana na upya wake, virusi hivyo vitakuwa changamoto kwa sababu miili ya watu itakuwa na uwezo mdogo au kutokuwa na uwezo kabisa wa kukabiliana navyo.

Tishio hilo jipya limekuja wakati dunia ikiwa bado inaendelea kupambana na janga la virusi vya corona ambavyo hadi sasa vimesababisha vifo zaidi ya 508,220 duniani kote.

Mara ya mwisho dunia kukumbwa na janga la mafua ilikuwa ni mwaka 2009 ambapo mafua ya nguruwe yalianzia nchini Mexico (A/H1N1pdm09), lakini hayakuwa na madhara makubwa kama ambavyo ilitazamiwa hasa kutokana na watu wazee kuwa na kinga ya mwili kutokana na ufanano wake na mafua mengi ambayo yalikuwepo miaka ya nyuma.

Aina mpya ya mafua iliyobainika nchini China ina ufanano kiasi na mafua ya nguruwe ya mwaka 2009, lakini kwa kiasi fulani yanatofautiana.

Send this to a friend