Vitu nane vinavyohitaji upate kibali cha kurusha drone Tanzania

0
116

Agosti 24, 2020 Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilitoa tangazo la kuwataka watu wote wanaomili ndege ndogo zisizo na rubani (drones) kuhakikisha zimesajiliwa ifikapo Agosti 28, 2020.

Tangazo hilo lilieleza sababu ya uamuzi huo ni utekelezaji wa kanuni za kiusalama za kufhibiti matumizi ya ndege zisizo na rubani ya mwaka 2018.

Akitolea ufafanuzi hilo, Mkurugenzi Mkuu s TCAA, Hamza Johari amesema kuwa “usajili wa drone ni USD 100 kwa mwaka. Hakuna kibali cha kurusha drone nchi nzima, ni kwa mkoa, hivyo kama umesajiliwa Dar es Salaam ukihitaji kwenda mkoa mwingine kikazi utakuja kuomba kibali tena.”

Ili kupata kibali, mhusika anatakiwa kuwa na nyaraka au taarifa mbalimbali ambazo ni:-

  1. Nakala za nyaraka za utambulisho wa mwombaji mfano, hati ya kusafiri, kitambulisho cha taifa, cheti cha kuzaliwa, leseni ya udereva au barua ya utambulisho kutoka Serikali za Mitaa.
  2. Anuani halisi inayoonesha makazi ya mwombaji, namba ya simu, barua pepe. Endapo muombaji ni taasisi au kampuni, ziwasilishwe nyaraka za usajili wake.
  3. Wasifu wa Mwombaji
  4. Muongozo wa mtumiaji (user manual) wa drone/UAV inayoombewa kibali ikionesha nchi ilikotengenezwa na vifaa vilivyopo katika ndege hiyo kama vile pay load types na uwezo wa camera.
  5. Kama drone/UAV hiyo imekodishwa zimambatanishwe nyaraka zote zenye maelezo ya ukodishwaji huo na muda wa matumizi yake.
  6. Nyaraka au cheti kinachoonesha uwezo wa mwendeshaji (operator) ndege hiyo.
  7. Kama mwombaji hana sifa au uwezo wa kurusha drone, ataje jina la mrushaji na iambatanishwe nakala ya cheti cha ujuzi wa atakayerusha.
  8. Maombi yote yataje eneo halisi litakalopigwa picha, tarehe ya kuanza na kumaliza urushaji na madhumuni ya urushaji.

Kanuni za udhibiti wa ndege hizo zinataka mtu au kampuni kuomba kibali kutoka TCAA kabla ya kuingiza na kusajili ndege hizo nchini.