Vodacom na SILABU washirikiana kuwezesha masomo mtandaoni

0
48

Katika jitihada za kujenga jamii ya kidigitali inayounganisha sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa ubunifu wa kiteknolojia, Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na SILABU wamezindua huduma itakayowarahisishia Watanzania kujifunza masomo na taaluma mbalimbali kwa ngazi tofauti nchini kwa njia ya mtandao muda na mahali popote walipo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika ofisi za Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Kamishna wa Elimu – Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Dr. Lyabwene Mutahaba amepongeza jitihada za Vodacom na SILABU kwa ubunifu wa huduma ya kujifunza mtandaoni inayoendana na mahitaji ya soko la elimu nchini na duniani kote kwa sasa.

“Elimu ya sasa haitulazimishi kuwepo moja kwa moja darasani ili tuweze kujifunza. Uwepo wa nyenzo za kidigitali unarahisishia wanafunzi na watu wa taaluma mbali mbali kujisomea na kujifunza kwa njia ya mtandao. Ongezeko la vifaa vya kidijiti kama simu janja, kompyuta na vishkwambi pamoja na miundominu ya intaneti vinaendelea kuwa chachu ya mapinduzi ya kidijitali katika sekta ya elimu. Niipongeze Vodacom kwa hatua hii kwani nimefahamishwa kuwa SILABU ni matokeo ya programu ya ‘Vodacom Digital Accelerator’, ambayo huzisaidia kampuni changa za kibunifu zinazotumia teknolojia kutatua changamoto zinazoikumba jamii yetu ya Watanzania,” alisema Dr. Mutahaba.

Kamishna wa Elimu – Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Dr. Lyabwene Mutahaba (kushoto) akipata maelekezo kutoka kwa Mwanzilishi Mwenza wa SILABU, Adam Duma (kulia) namna applikesheni ya SILABU inavyofanya kazi ambapo alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wake kuwawezesha wanafunzi na Watanzania kujifunza mtandaoni. Akifuatilia katikati ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania, Bi.Harriett Lwakatare, SILABU ni matokeo ya programu ya ‘Vodacom Digital Accelerator’, ambayo huzisaidia kampuni changa za kibunifu za kiteknolojia kutatua changamoto za kijamii.

SILABU, awali ikifahamika kama Smart Class ni mojawapo ya kampuni zilizoshiriki kwenye awamu ya kwanza ya programu ya Vodacom Digital Accelerator na kuibuka mshindi wa jumla ikiwakilisha sekta ya elimu ambapo kampuni hii changa ilijikita kwenye kuwaunganisha wanafunzi na wakufunzi ili kujifunza kwa njia ya mtandao.

“Ningependa kutoa rai kwa wanafunzi na Watanzania wote kutumia vema majukwaa haya ya kidigitali kuweza kujisomea na kujifunza masomo mbali mbali ambayo mengine hayapatikani darasani. Serikali inafanya jitihada kubwa kuweza kushirikiana na sekta binafsi na haswa makampuni ya mawasiliano na teknolojia kama vile Vodacom kuhakikisha huduma bora za mawasiliano zinawafikia Watanzania wote hasa wa vijijini ili nao waweze kushiriki katika uchumi wa kidigitali,” alimalizia Kamishna wa Elimu – Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia.

Akielezea kuhusu utekelezaji wa adhma ya Vodacom Tanzania ya kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali na kubadilisha maisha kupitia teknolojia, Mkurugenzi wa Huduma za Kidigitali wa Vodacom Tanzania PLC, Bw. Nguvu Kamando ameelezea kuwa SILABU ni uthibitisho tosha kuwa vijana wa Kitanzania wana bunifu zenye tija na wanaweza kufika mbali endapo wakipewa fursa na hamasa ya kuzitekeleza.

“SILABU ni moja wapo ya matunda kutoka kwenye programu yetu ya Vodacom Digital Accelerator (VDA) ambapo tunazishindanisha kampuni changa bunifu zinazotumia teknolojia kuleta mageuzi kwenye sekta ya elimu, afya, kilimo, usafiri, fedha, biashara za mtandaoni nk. Kwa mfano, mwanzoni mwa mwaka huu tuliendesha programu kwa mafanikio makubwa ambapo kampuni 12 zilizofuzu zilipata fursa ya kuwasilisha bunifu zao mbele ya majaji wabobevu. Kati ya hizo, kampuni tatu ziliibuka washindi ambapo mbali na zawadi ya fedha, watapata pia mafunzo zaidi ili kuwawezesha kusimama na kuanza kuwahudumia Watanzania kama hivi tunavyoona kwa SILABU leo hii,” alimalizia Bw. Kamando.

Kamishna wa Elimu – Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Dr. Lyabwene Mutahaba (kushoto) akipata maelekezo kutoka kwa Mwanzilishi Mwenza wa SILABU, Adam Duma (kulia) namna applikesheni ya SILABU inavyofanya kazi ambapo alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wake kuwawezesha wanafunzi na Watanzania kujifunza mtandaoni. Wakifuatilia wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Huduma kwa Wateja wa Vodacom Tanzania, Bi.Harriett Lwakatare, na Mkurugenzi wa Huduma za Kidigitali, Bw. Nguvu Kamando kutoka Vodacom Tanzania. SILABU ni matokeo ya programu ya ‘Vodacom Digital Accelerator’, ambayo huzisaidia kampuni changa za kibunifu za kiteknolojia kutatua changamoto za kijamii.

Naye kwa upande wake Mwanzilishi Mwenza wa SILABU, Adam Duma alihitimisha kwa kufafanua kuwa, “SILABU inatoa wigo mpana wa kujifunza kupitia madarasa yenye masomo yanayokidhi mahitaji ya ngazi tofauti za elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, Sekondari, Chuo Kikuu, pamoja na kozi zinazomuwezesha mtu kujiongezea ujuzi na maarifa.

Tunarahisisha uchaguzi wa madarasa yanayofundisha masomo tofauti kuendana na ratiba ya mtu. Pia tunawawezesha wanafunzi kuchagua namna ya kujifunza aidha mtandaoni au ana kwa ana na mwalimu, akiwa mwenyewe au kwa kujiunga kwenye kikundi na wanafunzi wengine. Niwahakikishie kwamba walimu na wakufunzi wote waliounganishwa kwenye mtandao wetu ni wabobevu na wamethibitishwa na mamlaka husika, hivyo wana ujuzi na uzoefu kwa mafunzo wanayoyatoa kuwasaidia wanafunzi na kuboresha uelewa na ufaulu wao.”

Send this to a friend