Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation imechangia kiasi cha shilingi Bilioni 2 kwaajili ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na kusambaa kwa janga la COVID – 19 nchini.
Akipokea mchango huo leo jijini Dar es salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ameishukuru Vodacom kwa mchango huo na kuhamasisha jitihada zaidi za hiari kwaajili ya kupambana na kusambaa kwa COVID – 19.
“Mpaka sasa watu 147 wamripotiwa wakiwa na virusi vya COVID-19. Watu 11 wamepona kabisa. Tunasikitika kutangaza watu watno waliofariki dunia. Kati ya watu 131 waliobaki, watu 127 wanaendelea vizuri na matibabu. Tumewaweka karantini kwasababu bado wana virusi vya COVID-19 ingawa hali zao ni nzuri.”
Akikabidhi hundi ya kiasi cha shilingi Bilioni 2 za kitanzania kwa serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, ambayo ni mfadhili mkuu wa taasisi hiyo, Ndugu Hisham Hendi amesema kuwa kampuni ya Vodacom imeshachukua hatua za awali za ndani na kwa jamii kwa ujumla kwa lengo la kusaidia juhudi za serikali katika kupambana na janga hili na kuhakikisha kazi na biashara zinaendelea.
“Vodacom Tanzania Foundation inachangia kiasi cha shilingi Bilioni 2 kusaidia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika juhudi zake za kudhibiti virusi vya corona katika ununuzi wa vifaa na vitendea kazi.
Vile vile tunatoa msaada wetu kwa ngazi zote za serikali ikiwemo Serikali Kuu, Serikali ya Zanzibar, Mikoa ya Tanzania bara na serikali za mitaa zinazofanya kazi moja kwa moja na wauzaji na wasambazaji walioidhinishwa na serikali katika kuwasilisha msaada unaohitajika; bila tozo la kodi ili kiwango chote cha fedha kiweze kupelekwa katika kuwanufaisha walengwa”.
Vodacom imechukua hatua ya makusudi katika kuhakikisha juhudi zake za kupambana na kusambaa kwa janga la virusi vya corona linafikia umma. Tumekuwa tunafanya kazi bega kwa bega na timu yako ya watendaji makini kupitia Wizara ya Afya kwa kutuma zaidi ya SMS milioni 100 kwa watumiaji wa simu waliojiandikisha walioko zaidi ya milioni 14. Watumiaji hawa wamejiandikisha kupokea ujumbe wa BURE wa taarifa na elimu kuhusu janga hili jambo ambalo linawawezesha kupambana na kusambaa kwa ugonjwa nchini Tanzania.
“Vodacom inaweza kuchukua nafasi muhimu katika kusaidia jamii wakati huu mgumu na imejidhatiti kufanya kila liwezekanalo katika wakati huu unaobadilika kwa kasi. Tutafanya jitihada za dhati kuweka mikakati ya kuhakikisha watanzania wanaendelea kuunganishwa na familia zao na marafiki na kuhakikisha kazi na biashara zinaendelea kwa kutumia teknlojia ya kufanya kazi nyumbani katika kipindi hiki kigumu kwa taifa.
Tunasisitizia utayari wetu na nia ya kuisaidia serikali na kufanya kila liwezekanalo kusaidia. Mafanikio yatategemeana na mwitikio wa wananchi na kuwajibika kwa pamoja kuzuia kisambaa kwa janga hili. Sote tuko katika janga hili.
Tunaamini kwamba juhudi zetu zitapokelewa vizuri kukusaidia wewe na serikali kwa ujumla katika kufikia mahitaji ya jamii tunayoitumikia, katika kipindi hiki kigumu.” Alihitimisha Ndugu Hisham.