Vodacom Tanzania Foundation yadhamini Mbio za Mbuzi 2023 zinazolenga ufadhili masomo elimu ya juu.

0
52

Dar es Salaam – Agosti 28, 2023. Katika kuunga mkono jitihada za upatikanaji wa fursa za kielimu nchini, Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, sehemu ya kampuni ya Vodacom Tanzania PLC iliyojikita katika shughuli za kijamii na kimaendeleo, imeingia ushirikiano na Rotary Club ya Oysterbay ambao ni waandaaji wa mbio za mbuzi (Goat Races) kama wadhamini wakuu ambazo zitafanyika Septemba 9 katika viwanja vya the Green Oysterbay kuanzia saa 6 mchana mpaka saa mbili usiku jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa kutangaza ushirikiano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Harriett Lwakatare amesema kuwa taasisi hii imejikita kwenye kutumia ubunifu kiteknolojia na mawasiliano kwa kushirikiana na taasisi za umma na sekta binafsi kusaidia jamii katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo nchini kote.

“Tangu kuanzishwa kwetu mwaka 2006 tumekuwa tukishirikiana kwa ukaribu na taasisi za umma na sekta binafsi, mashirika ya ndani na kimataifa kuungana mkono utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya serikali sehemu tofauti nchini. Miongoni mwa maeneo ambayo tumejikita zaidi ni sekta ya afya, elimu, mazingira, na uchumi jumuishi. Kwa upande wa elimu tunashirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na taasisi zake kama vile COSTECH, TEA, na Tanzania Data Lab kwenye miradi tofauti kama vile e-Fahamu au uungwanishwaji wa shule kwa kushirikiana na UCSAF pamoja na taasisi ya African Child Projects ambapo tunalenga kuzifikia shule 300 nchini kote,” alisema Bi. Lwakatare.

Aliendelea kwa kusema kuwa kwa kutumia mtandao mpana wa Vodacom na teknolojia yake ya mawasiliano iliyoenea nchini kote, wanatumia ubunifu wa teknolojia kubuni miradi na kuungana mkono iliyopo ili kuzinufaisha jamii ambazo nyingi huwa zinakuwa zinasahaulika.

“Ningependa kuwapongeza Rotary Club ya Oysterbay kwa ubunifu huu wa kipekee na jitihada zao za muda mrefu zinazokaribia miongo miwili sasa ambazo zimesaidia jamii kwa njia tofauti. Kwa namna ya kipekee wamefanikiwa kuwavutia washiriki katika mbio hizi, kufurahi lakini mapato yanayokusanywa yanarudishwa kwa jamii. Hii inaendana na dhamira tuliyonayo Vodacom kuhakikisha tunarudisha kwa jamii zinazotuzunguka ili kuwa na maendeleo kwenye sekta tofauti nchini. Ushiriki wetu kama mdhamini mkuu kwenye mbio za 2023 kwa mara ya kwanza unaonyesha kuamini juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika na faida yake kwa Watanzania,” aliongezea Bi. Lwakatare.

Kwa kumalizia, Mwenyekiti huyo wa bodi ya Vodacom Tanzania Foundation alisema kuwa, “kama mdhamini mkuu wa mbio hizi, tumechangia kiasi cha shilingi milioni 50 ambacho kitasaidia waandaaji katika shughuli mbalimbali za maandalizi. Lakini pia tutatumia mtandao wetu mpana kuwafahamisha wateja wetu, wadau, na Watanzania kwa ujumla kujumuika nasi kwa wingi siku ya tukio, tukifurahi kwa pamoja huku tukijua kuwa wanafunzi watakuwa na uhakika wa kuendelea na elimu yao ya masomo ya ngazi za juu kwa kulipiwa ada ili kufanikisha ndoto zao. Ningependa kutoa rai kwa washiriki wengi kujitokeza kwa wingi zaidi siku hiyo, pia kwa makampuni, taasisi, na mashirika mengine kuiga mfano kutoka kwa Dar Rotary Club kuja na ubunifu wa aina mbalimbali utakaowaleta Watanzania pamoja kwa maendeleo ya jamii nzima.”

Huu ni mwaka wa nne kwa ftotary Club ya Oysterbay kufanya mbio hizi kwa jina la The Goat Races, ambazo zinalenga kuvutia washiriki takribani 3,000. Kupitia mashindano haya kuwaleta watu pamoja ili kuchukua hatua kuhusu masuala muhimu zaidi duniani. Mwaka 2022 Mbio za Mbuzi za Rotary iilikusanya zaidi ya shiling milioni 246. Mapato yatakayopatikana mwaka huu yatatumika katika miradi mbali mbali ya kijamii kwa kuzingatia maeneo muhimu sita yaliyopewa kipaumbele na Rotary Club International na miradi ya mazingira ya Rotary Club ya Oysterbay, wanachama wake wa kujitolea pamoja na washirika wa ndani na kimataifa. Vipaumbele vya mwaka huu vitakua katika jitihada za kuwezesha, kupanua, na kutangaza miradi ya kijamii. Hii itahusisha miradi mipya, pamoja na miradi mingine inayo endelea kama vile misaada ya elimu, utoaji vifaa na elimu ya usafi, amani na usuluhishi wa migogoro, kujikinga na kutibu maradhi, maji na usafi, afya kwa wajawazito na watoto, elimu ya msingi, uchumi na maendeleo ya Jamii.

Rais wa Rotary Club ya Oysterbay 2023/24, Bw. Abdulrahman Hussein ameainisha kuwa mashindano ya mwaka huu yatakayokwenda kwa kauli mbiu ya “Celebrating the G.O.A.T. – the Greatest Of All Time”, kwa lengo la kuwakutanisha watu pamoja kuinufaisha jamii huku tukiwasherehekea watu ambao ni mifano na tunawaenzi.

“Tunashukuru kwa uaminifu tuliopewa na wadhamini wetu katika uwezo wa kutayarishaji tukio hili, na tunaamini Mbio za Mbuzi za mwaka 2023 zitakuwa burudani tosha kwa kila mtu,” alisema Bw. Hussein.

Naye kwa upande wake Meneja Miradi wa mbio za mwaka huu, Bw. Paul Muhato alimalizia kwa kusema, “mwaka huu mbio hizi zinaungwa mkono kwa kudhaminiwa na taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation ambao wanaungana nasi kwa mara ya kwanza. Tunashukuru kwa imani kutoka kwa wadhamini wetu wote ambao wengi wao wanajiunga nasi kwa mwaka mwingine wa ushirikiano. Tuna imani kuwa mbio za mwaka huu zitakuwa mojawapo ya mashindano makubwa zaidi.”

Send this to a friend