Vodacom Tanzania Foundation yaungana na waendesha baiskeli wa TwendeButiama kuadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation imetangaza ushirikiano na waendesha baiskeli mashuhuri wa TwendeButiama kama mdhamini mkuu wa tukio lao la kila mwaka la ziara ya Baiskeli inayoanzia jijini Dar es Salaam mpaka Butiama mkoani Mara. Tukio hili la uendeshaji wa baiskeli litakalodumu kwa siku 14, linatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe mosi mpaka 14 Oktoba mwaka huu, likitumika kama heshima ya maisha na kumbukumbu ya kumuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwl Julius Kambarage Nyerere, mtu muhimu katika historia ya Watanzania.
Gabriel Landa, Mwanzilishi Mwenza wa ziara ya TwendeButiama, ametoa shukran zake za dhati kwa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa udhamini wake. “Safari yetu ambayo ilianza mwaka 2018, inafanya Zaidi ya kuadhimisha kumbukumbu ya Baba wa Taifa; Tunahamasisha uendeshaji wa baiskeli – kitu ambacho Mwalimu alikipendelea zaidi – pamoja na kuwa vinara wa kusimamia masuala ambayo mwalimu aliyapambania kama vile elimu, utunzaji wa mazingira na afya bora. Kwa ushiriki wa sekta binafsi na ushirikiano wa waendesha baiskeli, wanaharakati wa mazingira na wataalamu wa afya, mchango wetu unalenga kuenzi maadili ya Mwalimu Nyerere,” alisema Landa.
Urithi wa tukio la TwendeButiama kwa miaka mitano sasa umekuwa ukiangazia masuala yanayogusa mazingira kwa kufanikisha kampeni ya upandaji miti zaidi ya 53,000. Kwa kuongezea, jitihada za kuchangisha fedha kupitia kampeni ya “Changia Dawati, Boresha Elimu” zinaonyesha kujidhatiti katika elimu, kuwezesha usambazaji wa madawati takribani 200 katika shule za msingi sita zilizoko mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma na Mara.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa Habari, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah amesema kuwa, “tunayo furaha kubwa kuujulisha umma kuwa tunashirikiana na ziara ya Baiskeli ya TwendeButiama kama mdhamini mkuu kwa mwaka huu. Ushirikiano huu ni zaidi ya udhamini; ni muunganiko wa maadili, kujitolea, na kujidhadhatiti kuitumikia jamii ya Kitanzania kwani kipindi cha ziara tutajihusisha na shughuli mbalimbali zinazolenga kuendeleza na kuenzi kumbukumbu ya maisha ya Mwalimu Nyerere.”
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah. (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutangaza rasmi udhamini wa msafara wa waendesha baiskeli wa ‘Twende Butiama’ kwa ajili ya kuenzi Maisha na kumbukumbu ya hayati baba wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Wakimsikiliza kulia ni Mwenyekiti wa Msafara wa Twende Butiama, Gabriel Landa na kushoto ni Mhariri wa ITV, Capital TV na Radio One, Amri Masare, msafara wa waendesha baiskeli utaanza Oktoba mosi Msasani, Dar es Salaam nyumbani kwa Mwalimu Nyerere na kumalizika Oktoba 14 Wilayani Butiama.
Mbali na kuchangia garama zote za uendeshaji wa ajili ya msafara huu kuelekea Butiama, Vodacom Tanzania Foundation imejipanga kushiriki kwenye shughuli tofauti zinazoendana na mkakati wao wa kuleta mabadiliko kwa kuboresha huduma za afya, upatikanaji wa elimu bora na uwezeshaji wa kiuchumi kwa garama ya zaidi ya millioni 200.
“Tutaungana na waendesha baiskeli wa TwendeButiama kuchangia madawati katika shule 5 na kupanda miche ya miti zaidi ya 4,000 katika mikoa tofauti ambayo waendesha baiskeli watapita. Shughuli hii inaendana na mkakati wetu wa kupanda miti milioni 2 nchini kote ifikapo mwaka 2030. Kwa kuongezea, tunashirikiana na ‘Afya Checkers’ ambao ni wataalamu wa huduma ya afya kuandaa kambi maalum zitakazotoa huduma ya upimaji, matibabu ya bure na pia kuwapa rufaa wagonjwa katika maeneo ya Mwanza, Bunda, na Butiama ikiwa ni juhudi zetu za kupambana na magonjwa ya kuambukiza nchini, vilevile tutachangia vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama,” alisema Bi. Farah.
Kwa upande wake Dr. Romana Malikusema akizungumza kwa niaba ya wataalamu wa afya ambao watakuwa sehemu ya ufanikishaji wa Kambi ya Matibabu ya bure ameishukuru Vodacom Tanzania Foundation kwa kuwaunga mkono kuhakikisha zoezi la kambi hizo linafanikiwa kwa wakazi wa Mwanza, Bunda na Butiama.
“Tunayofuraha kuwa sehemu ya ziara ya Baiskeli ya TwendeButiama kuenzi kumbukumbu ya Mwalimu kupitia uwezeshaji wa kambi ya matibabu ya bure. Mwalimu Nyerere alijitolea kupambana na magonjwa nchini Tanzania na tunatarajia kusaidia na kuwahudumia watu wengi kadri tuwezavyo. Tutakuwa wataalamu wa afya kama manesi, madaktari na wataalam wa lishe watakaowahudumia na kuwashauri watu ambao watahudhuria. Ningependa kutoa wito kwa washirika wengi Zaidi kujitokeza ili kuunga mkono jitihada hizi za kipekee zinazolenga kugusa Maisha ya watu wengi Zaidi,” aliongeza Dkt Malikusema.
Kwa taarifa zaidi kuhusu ziara hii, tafadhali tembelea (http://www.twendebutiama.com).
Kuhusu Vodacom Tanzania Foundation
Vodacom Tanzania Foundation ni sehemu ya Vodacom Tanzania PLC iliyojikita katika miradi ya kusaidia jamii kwa kutimiza wajibu wake wa kuunufaisha umma hususani makubdi yasiyojiweza hususani wanawake na vijana. Taasisi inajumuisha misaada ya kijamii kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi kutoa ufumbuzi kwa changamoto mbalimbali za kijamii.
Kwa kufanya kazi na taasisi za ndani zisizo za kiserikali na washirika, mpaka sasa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation imeunga mkono zaidi ya miradi 120 kwa kuwekeza zaidi ya TZS 15 bilioni kuboresha Maisha ya Watanzania.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali tembelea:
https://vodacom.co.tz/en/vodacom_foundation_aboutus/?SID=1u5nsmti8ahqks35k9tds71652