Vodacom: Wateja wanaofanyiwa utapeli waripoti kwetu mapema

0
9

Kampuni ya Vodacom Tanzania imesema katika ukuaji wa mitandao na teknolojia, Watanzania wengi wanalizwa zaidi na udanganyifu shirikishi (social engineering) ambapo matapeli humfanya mtu atoe taarifa zake binafasi au kumlazimisha kwa namna ya kirafiki kutumia hisia zake kuwezesha kukamilisha kitendo cha utapeli.

Akizungumza katika mahojiano katika kipindi cha Leo Tena cha Clouds FM, Mtaalam wa Uchunguzi wa Udanganyifu wa Kiforensiki kutoka Vodacom, Rona Katuma amesema kuna njia kuu nne ambazo zinatumiwa na matapeli ikiwemo kutumia ujumbe, kupiga simu na kujifanya mhudumu wa mitandao ya simu, njia ya ana kwa ana ambapo matapeli hujifanya watoa huduma mitaani na kufanya udanganyifu na njia nyingine ni kutumia online.

“Sisi kama Vodacom tunawajali sana wateja wetu na tunawapenda, tunataka kuwakumbusha na kuwasisitiza kwamba pale wanapoona kwamba ametapeliwa iwe ni kupitia mtandao wetu wa Vodacom au mtandao wowote, sisi Vodacom kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano, tuna njia ya kuripoti utapeli hata kama wewe unaona hapatikani, huwezi kupiga simu, basi unaweza ukatumia simu ya mtu yeyote kuripoti utapeli.

Iwe umetapeliwa kwa kupigiwa simu au tapeli hajafanikiwa kukutapeli na umeweza kumgundua au umepata ujumbe wowote wa kitapeli, tunakushauri uripoti kwetu kupitia 15040. Unachotakiwa kufanya ni kuutuma ule ujumbe kwenye 15040 kisha utaweka namba ya huyo tapeli, sisi tutashughulika na ile namba kwa ku-block NIDA yake anayosajilia, ku-block IMEI, na ku-block hiyo namba ya simu,” ameeleza.

Amesema endapo mwathirika atatoa taarifa mapema inasaidia mamlaka ya simu kuzuia pesa kuhamishwa na tapeli, na mteja anaweza kurejeshewa pesa zake baada ya uchunguzi wa Polisi.

Kwa upande wa Mkaguzi Msaidi wa Polisi, Waziri Makang’ila amewatoa hofu wananchi na kuwasisitiza kuripoti polisi pindi wanapoibiwa simu zao ili ufanyike uchunguzi zaidi na kuwabaini wahalifu.

Send this to a friend