Vodacom yashirikiana na NMB, Google kurahisisha upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu kupitia mikopo ya simu

0
47

Ushirikiano mpya kati ya Google, NMB na Vodacom Tanzania Plc unatarajiwa kuimarisha mapinduzi ya kidijitali kwa kuwezesha upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu nchini. Kwa kulipa kiasi cha kuanzia cha Shilingi 20,000, wateja wa Vodacom wanaotimiza vigezo watapata simu janja zinazoweza kutumia mtandao wa 4G na hivyo kuwawezesha kunufaika na fursa zinazopatikana mtandaoni.

Mpango huo mpya uitwao “Miliki Simu, Lipa Mdogo Mdogo” kwa ushirikiano NMB na Android (mfumo wa uendeshaji wa Google kwa vifaa vya mkononi) unaenda sambamba na dira ya serikali ya ujumuishi wa kidijitali.

Mkurugenzi wa Fedha wa Vodacom Tanzania PLC, Bi. Hilda Bujiku (kushoto) akiwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMBBw. Filbert Mponzi (kulia) wakifurahia kwa Pamoja baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa kampeni ya Miliki Simu, Lipa Mdogo Mdogo” kwa kushirikiana na kampuni ya Google jijini Dar es Salaam leo. Kampeni hii inawawezesha Watanzania upatikanaji wa simu janja kwa bei nafuu nchini kwa kulipa kiasi cha kuanzia cha Shilingi 20,000 na kulipia kidogo kidogo kwa kima cha chini cha kuanzia shilingi 900 kuimarisha adhma ya serikali ya mapinduzi na ujumuishi wa kidigitali. 

“Maono yetu daima yamekuwa kuipeleka Tanzania kwenye ulimwengu wa kidijitali na kubadilisha maisha kupitia teknolojia, kwa hivyo ushirikiano huu unaenda sambamba na adhma yetu ya kuwafungulia wateja wetu fursa zinazobadilisha maisha. Tunaamini kwamba ushirikiano huu utaleta mageuzi katika upatikanaji wa simu janja kwa wale ambao bado hawajanufaika na zana hizi za kidijitali. Tumeazimia kuwezesha wateja milioni moja kumiliki simu janja zenye uwezo wa 4G katika mwaka huu wa fedha pekee, na hivyo kuchangia kupunguza pengo kati ya wanaotumia na wasiotumia intaneti nchini” alisema Bi. Hilda Bujiku, Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni ya Vodacom Tanzania.

Mikopo ya simu ni mbinu inayowezesha umiliki wa simu janja kirahisi na kwa gharama nafuu kupitia malipo ya siku au ya wiki kwa kima kidogo cha hadi Tsh 900 huku mtumiaji akifurahia manufaa yanayokuja na kuunganishwa kidijitali. Ushirikiano huu utatumia uwezo mpya wa kipengele cha kusimamia vifaa kwenye mfumo wa uendeshaji wa Android.

“Lengo la Android daima limekuwa kuwawezesha watu kupitia huduma za kikompyuta. Ufikiaji wa fursa zilizo kwenye intaneti ni muhimu sana kwa ukuaji wa kiuchumi na ujumuishaji wa kijamii katika nchi yoyote ile. Tunaamini kwamba ushirikiano huu utawaleta Watanzania wengi mtandaoni na kuwasaidia kutumia fursa zinazopatikana mtandaoni,” amesema Martin Njoroge, Mkuu wa Android wa Ushirikiano wa Kimajukwaa, Afrika Mashariki.

Kwa upande wa Benki ya NMB, Bw. Filbert Mponzi, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki hiyo alisema “Ubia huu wenye tija ni sahihi kabisa kwani Vodacom itawapatia wateja wake mpango wa kulipia simu janja hivyo kuwezesha kupanda daraja na kumiliki simu janja kupitia malipo ya awamu hivyo kufungua uchumi wa kidijitali na kutengeneza fursa za ziada kwa Watanzania. Vile vile, ubia huu unaenda sambamba na ajenda yetu ya ujumuishwaji wa kidijitali al maarufu Teleza Kidijitali”

Kufurahia huduma hii, wateja wa Vodacom watatakiwa kupiga *150*00# > 5 > 5 > 1 # ili kuona kama wanakidhi vigezo na hivyo kujiunga kwenye huduma, baada ya hapo watapokea SMS iliyo na namba ya kumbukumbu. Wateja watachukua simu zao katika maduka ya Vodacom baada ya kulipa kianzio cha hadi Shilingi 20,000. Vodacom itawazawadia wateja wake MB 100, dakika 10 za kupiga mitandao yote na SMS 10 zitakazotumika ndani ya masaa 24 pindi watakapokamilisha marejesho kwa wakati. Iwapo mteja hatafanya marejesho kwa wakati, Vodacom itafunga kifaa hicho. Hali kadhalika, hata wakati simu imefungwa mteja bado ataweza kuwasiliana na huduma kwa wateja, kutumia M-PESA pamoja na aplikesheni ya Kiosk.

Kwa maelezo zaidi kuhusu Miliki Simu, Lipa Mdogo Mdogo, wateja wa Vodacom wanahimizwa kubonyeza *150*00# > 5 > 5 > 6 au kupiga namba ya huduma kwa wateja kupitia nambari 100 ili kupata maelezo zaidi.

Send this to a friend