Vodacom yatambulisha eSIM, kadi ya simu ya kielektroniki iliyo rafiki kwa mazingira.

0
73

Kampuni ya teknolojia na mawasiliano inayo ongoza nchini, Vodacom Tanzania PLC imewataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kuwa sasa wanaweza kuhamia kwenye kadi za kielektroniki yaani eSIM zinazopatikana kwenye mtandao supa wa Vodacom. Laini hii ambayo inafanya kazi sawa na kadi za sasa ni rafiki kwa mazingira kwani huunganishwa moja kwa moja kielektroniki kwenye vifaa vinavyokubali matumizi yake, hivyo havitegemei kuzalishwa kwa kutumia plastiki.

Akizungumza wakati wa hafla ya utambulisho huo, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania, Bi. Linda Riwa amebainisha kuwa kuletwa kwa kadi hizi mpya kunaenda sambamba na ari ya kampuni hiyo, ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ulimwenguni, kukidhi mahitaji ya wateja wake na kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.

“Kuongezeka kwa matumizi ya simujanja kunapelekea uhitaji wa teknolojia zilizoendelea zaidi na ndio maana leo tunatambulisha kwenu huduma hii. Najua wengi wenu mtakuwa mnajiuliza kwanini mbadilishe kadi mlizonazo endapo eSIM tunayoitambulisha leo inafanya kazi sawa na kadi za sasa. Jibu ni rahisi, eSIM inakuwezesha kuwa na namba zaidi ya moja kwenye simu yako hivyo utaweza kubadilisha mitandao pasipo kuhitajika kutoa kadi ya simu. Vile vile, kwa kuwa eSIM inaunganishwa moja kwa moja kwenye simu yako basi si rahisi kupotea au kuharibika na ni chaguo lilio rafiki kwa mazingira,” alielezea Bi. Riwa.

Mkurugenzi huyo wa Biashara aliongeza kuwa mteja yeyote wa Vodacom mwenye simujanja yenye uwezo wa kutumia eSIM anaweza kutembelea maduka ya Vodacom ili kubadilishiwa laini yake.

“Kuna njia mbili za kutambua kama simu yako ina uwezo wa kutumia eSIM; ya kwanza ni kwa mteja kupiga namba *#06# na kisha utaona namba nyingi zenye lebo za IMEI, ICCID na EID. EID ni kitambulisho kuwa simu ina uwezo wa matumizi ya eSIM. Njia ya pili ni kupitia menu ya simu kwenye Settings ambapo kwa watumiaji wa Android wataipata kwa kwenda kwenye Settings > Connections > SIM Manager > hapa itaonyesha eSIM. Kwa upande wa watumiaji wa iPhone, wataenda kwenye Settings > Mobile Data > Hapa itaonyeha Add eSIM” alimalizia Bi. Riwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Vodacom Business wa kampuni hiyo, Bw. Arjun Dhillon aliongezea kwa kusema kuwa, “eSIM ni suluhisho sahihi sio tu kwa wateja wa kila siku bali pia wale wasafiri, wafanyabishara na watu wa maofisini wanaosafiri mara kwa mara. Hii ni kwasababu pale wanaposafiri kwenda ng’ambo, hawatakuwa na hofu ya kupoteza laini zao za simu pale wanapolazimika kutumia kadi za nchi waliyoko kwani eSIM yao tayari itakuwa imeunganishwa kwenye simu kielektroniki. Hata kwa watalii wanaotembelea Tanzania, wataweza kujiunga kwenye mtandao wetu kirahisi kwani usajili wa eSIM ni rahisi na wa haraka hivyo kuwawezesha kuendelea kuunganishwa kimawasiliano na wapendwa wao

“Tutatendelea kushirikiana na makampuni yanayozalisha simujanja ili kuwapa wateja wetu suluhisho za kidijitali pamoja na vifaa vya kisasa vikiwemo vile vyenye uwezo wa kutumia teknolojia ya eSIM tunayoitambulisha leo na hii ndio maana Vodacom tunasema Pamoja Tunaweza,” alifafanua Bw Dhillon.

Send this to a friend