Vodacom yatoa tuzo ikitimiza miaka 11 bila vifo kazini ikitumia ubunifu

0
42

Kampuni ya Teknolojia na mawasiliano, Vodacom Tanzania PLC imewapongeza kwa kuwapatia tuzo mbalimbali washirika na watoa huduma wake kwa kuzingatia viwango vya usalama kwa kutumia teknolojia mahali pa kazi na kupelekea kutotokea kwa kifo chochote kwa takribani miaka 11 sasa.

Kampuni hiyo iliendesha hafla fupi ya utoaji wa tuzo na vyeti vya shukran katika vipengele vinne vikiwemo Usalama wa Barabarani, Ubunifu wa Kidigitali katika Usalama na Afya, Usimamizi na Ukaguzi mahala pa kazi, pamoja na Usimamizi na Utoaji wa taarifa za Ajali wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania PLC, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (wa pili kulia) akimkabidhi cheti cha Ubunifu wa Kidigitali katika Usalama na Afya, Zhang Long (wa pili kushoto) kutokea Huawei Tanzania wakati wa hafla ya kutoa tunzo kwa washirika na watoa huduma wa kampuni hiyo wiki iliyopita jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire.   

Akizungumza wakati wa kukabidhi vyeti na tuzo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania Plc, Jaji Mstaafu Thomas B. Mihayo alifafanua umuhimu wa kuainisha ajenda ya usalama na afya kwenye mazingira ya kufanyia kazi, “kila mmoja wenu anao mchango mkubwa kwenye mafanikio ya Vodacom. Kujitoa kwenu, kuzingatia taaluma na kutuunga mkono kwa uthabiti katika kusimamia nguzo hizi kumepelekea mafanikio haya. Kwa kuongezea, milango yetu ipo wazi kupokea maoni, mapendekezo na kushirikiana kwenye jitihada za kujenga mustakabali imara na endelevu zaidi kwa siku zijazo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc, Philip Besiimire alibainisha kuwa, “kama kampuni inayojiendesha kiteknolojia, tunazingatia kwa kiasi kikubwa umuhimu wa ubunifu wa kidigitali katika kuboresha shughuli za kiafya na usalama mahala pa kazi, tukizifanya sehemu za kufanyia kazi kuwa salama zaidi na kupunguza hatari ya ajali na majeruhi. Ubunifu wa aina hii ni muhimu katika kupunguza hatari na ajali kwa washirika na watoa huduma wetu.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania PLC, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (wa pili kulia) akimkabidhi tuzo ya Usalama wa Barabarani, Atilio Lupala (wa pili kushoto) kutoka Talent Solutions wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa washirika na watoa huduma wa kampuni hiyo wiki iliyopita jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire na wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Kwa kutambua changamoto mbalimbali zinazoambatana na shughuli zake, Vodacom Tanzania Plc inatambua mchango wa watoa huduma wake ambao wanapitia mazingira tofauti ya hatari mara kwa mara ili kuhakikisha ufanisi wa uendeshaji wa huduma za mtandao, na tuzo hizi zinatoa fursa ya kuwapongeza kwa kuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha usalama kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Kwa miaka mingi, Vodacom imekuwa kinara kwenye kutambua umuhimu wa viwango vya ubora katika mnyororo wa utoaji huduma zake, na kupelekea kufanikinisha kuwa na miaka 11 mtawalia bila ya vifo mahala pa kazi. Mwaka jana, kampuni hiyo iijivunia kupokea ujumbe kutoka kampuni za Safaricom Kenya na Safaricom Ethiopia waliokuja kujifunza na kupata uzoefu wa Vodacom Tanzania Plc wa kufanikisha miaka kumi bila ya vifo huku ikitumia ubunifu wa kidigitali kwenye masuala ya afya na usalama.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania PLC, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji, Philip Besiimire (kulia), wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kenneth Ngugi (aliyeshikilia tuzo) kutoka kampuni ya Power Group baada ya kuibuka washindi wa kipengele cha Uratibu na Ukaguzi mahala pa kazi wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa washirika na watoa huduma wa kampuni hiyo wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

 

Send this to a friend