Vodacom yazindua mikopo ya kidijitali kupitia kampeni ya ‘Maisha ni Kujiongeza na M-Pesa’ kwa ajili ya wateja na wafanyabiashara

0
57
  • Yatambulisha mikopo mbali mbali ikiwemo  mikopo mipya ya Chomoka na ada ya bima kwa wamiliki wa vyombo vya moto, mikopo kwa wafanyabiashara, mawakala, wateja binafsi ikiwemo mikopo nafuu ya simu janja.  

Kampuni ya teknolojia na mawasiliano, Vodacom Tanzania PLC, kupitia huduma yake ya M-Pesa, imezindua kampeni ijulikanayo kama ‘Maisha ni Kujiongeza na M-Pesa’ inayowalenga wateja, mawakala, madereva wa vyombo vya moto, na wafanyabiashara nchini kote ambao watanufaika kupitia huduma zake za mikopo mpya na zilizoboreshwa kama vile M-Pawa, Songesha, Wakala Songesha, Wezesha Wakala ili kukidhi mahitaji yao kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi ya kidigitali nchini na duniani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa M-Pesa, Bw. Epimack Mbeteni amesema kuwa kwa miaka 15 sasa M-Pesa imekuwa bega kwa bega na Watanzania kwenye safari ya kurahisisha na kuleta mapinduzi ya huduma za kutuma na kupokea pesa kupitia simu za mkononi ambapo mpaka sasa ina watumiaji zaidi ya milioni 17 kama inavyoripotiwa na TCRA.

“Leo tunayofuraha kuwajulisha Watanzania kuwa tumepanua wigo wa huduma zetu za akiba na mikopo zinazopatikana kupitia M-Pesa. Ya kwanza ni Mgodi, hii ni huduma ya kifedha ambayo inatoa fursa kwa wateja wa Vodacom kujiwekea akiba na kupata mikopo kupitia simu zao za mkononi wa kiwango cha kati wa mpaka kufikia siku 30. Pili, tunatambulisha kwenu mikopo mahususi kwa wamiliki na madereva wa vyombo vya moto na hii ni Chomoka pamoja na Mkopo wa Ada ya Bima. Kupitia Chomoka dereva ataweza kupata mkopo wa mafuta kwenye kituo chochote cha mafuta nchini chenye huduma ya LIPA kwa SIMU wakati mkopo wa ada wa bima utamuwezesha kukamilisha malipo ya bima endapo amepungukiwa pesa au hana kabisa. Lengo ni kuwawezesha kuendelea na shughuli zao kwa usalama na kuokoa muda zaidi,” alisema Bw. Mbeteni.

Katika kuunga mkono jitihada za serikali kupunguza pengo liliopo katika matumizi ya simu janja zinazochochea ukuaji wa matumizi ya intaneti na uchumi wa kidijitali, Vodacom pia ilitambulisha huduma ya mikopo nafuu kwenye vifaa hivyo ambapo kwa malipo ya awali ya shilingi 20,000/- mteja ataweza kumiliki simu janja na kulipa kidogo kidogo kwa kima cha chini cha kuanzia shilingi 900/- kwa siku.

Mkurugenzi wa M-Pesa aliendelea kufafanua kuwa wamefanya maboresho ya huduma zao zingine kwa kusema, “tumeboresha huduma ya Songesha ambayo ni msaada mkubwa katika kukamilisha miamala tofauti tofauti kwa wateja binafsi. Sasa mteja anaweza kusongesha mara nyingi vile vile akarudisha kiwango alichokopa na kusongesha tena mpaka kufikia kiwango anachoruhusiwa. Hii inamaanisha kuwa tumeongeza kiwango cha mteja kusongesha kwa 20% na kama hiyo haitoshi sasa mteja ataweza kusongesha mpaka vifurushi kupitia menu ya USSD ambayo ni *149*01# na sio lazima asongeshe vifurushi kwa njia ya M-Pesa pekee kama ilivyokuwa hapo awali.”

“Kupitia M-Pawa, sasa mteja hahitaji tena kuweka akiba ndipo apatiwe mkopo, ingawa ukiweka akiba uwezekano wa kupata kiwango cha juu ni mkubwa zaidi. Hadi sasa, wateja wapya takribani 400,000 wanaweza kufurahia huduma hii kwa mara ya kwanza. Cha kuzingatia ni kwamba tunaangalia tabia na mwenendo wa mteja ili kuweza kuongezewa kiwango cha mkopo kutoka M-Pesa kwa kila mwezi,” aliongezea bwana Mbeteni.

Kampeni hiyo pia imetambulisha Mikopo ya Biashara kwa wafanyabiashara waliosajiliwa na M-Pesa kupitia huduma ya LIPA ambapo watajipatia mikopo kutokana na viwango vya miamala wanayoifanya na idadi ya wateja walionao. Hii itawasaidia kujiongezea mtaji na vile vile kuimarisha uendeshaji wa biashara zao. Hata hivyo kampeni hii haijawaacha Mawakala nyuma kwani kupitia Wezesha Wakala mawakala wanaweza kujipatia mkopo wa biashara na hii imeboreshwa kwa kuongeza kikomo cha mkopo kwa hadi asilimia 100 hivyo kuwawezesha mawakala kutumia fedha hizi kugharamia biashara zao zingine mbali na uwakala. Hadi sasa, zaidi ya mawakala 76,000 nchi nzima wananufaika na huduma hii. Hali kadhalika, Wakala Songesha ambayo ni huduma inayowawezesha kupata mikopo ya floti bila riba imeboreshwa kwa kuongeza maradufu kikomo cha Songesha kwa mawakala wote.

Bw. Mbeteni alimalizia kwa kusema “kama mnavyojua maisha ni safari ya maendeleo endelevu. Sisi sote tuna uwezo wa kukua na kufikia malengo yetu lakini ili kufanikisha hili, tunahitaji kuwa na maono ya kile tunachotaka kufikia. Tunahitaji pia kupata washirika sahihi ambao watatuunga mkono katika safari yetu. M-Pesa ndiye mshirika huyo. Ila pia kama M-Pesa hatufanyi hili peke yetu bali tuna washirika wetu wanaotuwezesha. Kwa upande wa kibiashara tunao Finca Microfinance Bank, NCBA Bank, Mwanga Hakika Bank, DTB Bank na NMB Bank. Vile vile tuna washirika wanaounganisha teknolojia zetu na mabenki ambao ni Kuunda na Credable.”

Send this to a friend