Vodacom yazindua mnara wa mawasiliano Makunduchi, Zanzibar

0
62

Katika kuunga mkono azma ya serikali ya kupanua na kuimarisha huduma za mawasiliano nchini kote, kampuni ya teknolojia na mawasiliano ya Vodacom Tanzania leo imezindua mnara wa mawasiliano katika mji wa Makunduchi, uliopo ndani ya Mkoa wa Kusini Unguja.

Mkurugenzi wa Wakala wa Mkongo Zanzibar (ZICTIA), Bw. Shukuru Awadh Suleiman (katikati) pamoja na Mkuu wa mauzo wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania PLC, Bi. Brigita Shirima (wa pili kulia) wakikata utepe wakati wa uzinduzi wa mnara wa mawasiliano wa Vodacom Tanzania katika mji wa Makunduchi uliopo ndani ya Mkoa wa Kusini Unguja jana. Pamoja nao wakati wa uzinduzi ambao ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kuunga mkono azma ya serikali ya kupanua na kuimarisha huduma za mawasiliano nchini kote. Kutoka kushoto ni Meneja Mauzo Mwandamizi Liston Chale, Katibu Tawala Wilaya ya Kusini – Unguja, Baraka Omary Kaengeo na kulia ni Meneja Mauzo Fadhili Linga.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mnara huo mgeni rasmi Bw.Shukuru Awadh Suleiman Mkurugenzi wa Wakala wa Mkonga Zanizibar (ZICTIA) aliipongeza Vodacom kwa kuiunga mkono serikali katika kufikisha huduma za mawasiliano na intaneti kila kona ya nchi hususan vijijini ambapo wananchi wengi bado hawajafikiwa.

“Nimefurahi kuwa uzinduzi wa leo unafanyika wakati si muda mrefu umepita tangu utiaji saini wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali ulioshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma. Katika hotuba yake, Mh. Rais aliwataka watoa huduma za mawasiliano kuyapa kipaumbele maeneo ya vijijini, akisisitiza kuwa maeneo hayo yana watu wengi hali kadhalika yamesahaulika kwa muda mrefu. Aidha alibainisha kuwa kuboreshwa kwa mawasiliano kutachochea sekta mbalimbali za kiuchumi zikiwemo afya na kilimo ambazo ni msingi kwa maendeleo ya nchi yetu.” alinukuliwa Bw.Suleiman.

“Nawapongeza Vodacom kwa uzinduzi wa mnara huu kwani utasaidia wakazi wa Makunduchi kupata huduma za mawasiliano zenye ubora na uhakika. Aidha wakazi wa Makunduchi na maeneo ya jirani watanufaika kwa kiasi kikubwa na huduma zenu mbalimbali kama bidhaa za kidijitali pamoja na zile pesa mtandao kupitia M-Pesa hivyo kuongeza kasi ya ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo na uvuvi. Niwaombe wakazi wa Makunduchi na maeneo ya jirani kutunza vyema miundombinu hii muhimu na kuchangamkia fursa zinazoambatana na uwepo wake,” alimalizia Mkurugenzi huyo.

Vodacom Tanzania ndiyo kampuni inayoongoza kwenye sekta ya mawasiliano nchini ikijivunia zaidi ya wateja milioni 18. Vile vile kampuni hii ilikuwa ya kwanza kutambulisha mtandao wa 5G hivyo kuiweka Tanzania kwenye ramani inapokuja ya kimataifa katika maswala ya teknolojia ya mawasiliano. Aidha, huduma yake ya kifedha kwa njia ya simu ijulikanayo kama M-Pesa imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa ushirikishwaji wa kifedha nchini kwa miaka 15.

Kwa upande wake Mkuu wa Kanda ya Dar na Pwani wa Vodacom Bi.Brigita Shirima alisisitiza kuwa ujenzi wa minara ya mawasiliano nchini unakwenda sambamba na uwekezaji unaoendelea ili kuwahakikishia wateja wao wanapata huduma za uhakika na zenye ubora popote walipo.

“Vodacom inajivunia kutoa huduma za mawasiliano kwa zaidi ya miaka 20 nchini Tanzania. Tunaendelea kupanua na kuboresha miundombinu ya mtandao wetu kwa kuzingatia huduma za 4G na 5G ili kuhakikisha wateja wetu wanashiriki kikamilifu katika mapinduzi ya nne ya viwanda. Aidha, kupitia huduma zetu za kifedha kwa njia ya simu, tunaendelea kuvumbua na kuimarisha huduma ya M-Pesa hivyo kukidhi mahitaji zaidi ya kuweka akiba na kukopeshana bali pia kuwezesha uhamisho wa fedha ndani na nje ya nchi huku tukitengeneza fursa za ajira kupitia mtandao wetu mpana wa mawakala” aliongeza Bi. Shirima.

Wakati wa hafla ya uzinduzi wa mnara wa Makunduchi, ilibainaika kwamba mbali ya mnara huo unaozindulkiwa, Vodacom imekamilisha minara mingine mitatu siku za hivi karibuni, ambayo yote tayari iko hewani na mingine miwili iko kwenye hatua za mwisho. Hii inakwenda kuonyesha uwekezaji endelevu wa Vodacom na dhamira yake ya kuimarisha huduma za mawasiliano visiwani Zanzibar.

Mkuu wa Kanda ya Dar na Pwani alihitimisha kwa kusema, “Uwekezaji huu unaoendelea katika miundombinu ya mawasiliano ni kwa manufaa mapana ya jamii zetu na ni matumaini yetu kuwa utachochea ukuaji zaidi wa shughuli za kijamii na kiuchumi.” Alimalizia kwa kuishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi kwa makampuni kama Vodacom hivyo kuwaruhusu kuendelea kuwekeza nchini.

 

Send this to a friend