Vodacom Yazindua Twende Butiama 2025 kwa Lengo la Kuboresha Elimu, Afya na Mazingira

0
5

Kwa miaka ishirini na tano, Vodacom Tanzania PLC imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuchochea maendeleo endelevu katika jamii. Msafara wa Twende Butiama wa mwaka 2025 kwa mara nyingine unadhaminiwa na Vodacom na litahusisha msafara wa umbali  wa karibu kilomita 1,500 likipita katika mikoa 11 kuanzia tarehe 3 hadi 13 mwezi Julai, na kumalizika kwa kishindo katika kijiji cha Butiama mkoani Mara – mahali alipozaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akizungumzia kuhusu msafara huo, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania na Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Zuweina Farah, alisisitiza dhamira ya kampuni hiyo kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika harakati za maendeleo nchini.

Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania Bi. Zuweina Farah, akizungumza wakati wa uzinduzi wa msafara wa Vodacom Twende Butiama kwa mwaka 2025. Kushoto ni Mwanzilishi wa Twende Butiama, Bw. Gabriel Landa. Msafara huo utakaofanyika mwezi Julai kutoka Dar es Salaam mpaka Butiama unalenga kuenzi fikra za Baba wa Taifa hayati Mwl Julius K. Nyerere ambazo ni kuboresha elimu, afya na mazingira na unadhaminiwa na kampuni hiyo. Mkutano huo umefanyika jijini Arusha tarehe 15 mwezi Aprili 2025.

“Tunaamini katika kuunganisha Watanzania kwa mustakabali bora, na Twende Butiama ni moja ya njia tunayoitumia kutimiza dira hiyo. Iwe ni ujumuishaji wa kidijitali, upatikanaji wa elimu, huduma bure za afya au utunzaji wa mazingira, kampeni hii inaonesha nguvu ya ushirikiano na dhamira ya kweli,” alisema Zuweina.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Twende Butiama imeboresha maisha ya maelfu ya Watanzania. Zaidi ya watu 150,000 wamenufaika na huduma za afya bure, zaidi ya miti 100,000 imepandwa katika shule mbalimbali nchini na kuhamasisha uelewa wa mazingira na kuboresha mazingira ya kujifunzia, zaidi ya madawati 1,900 yamegawiwa kwa shule za msingi 34 ili kupunguza idadi ya wanafunzi kukaa chini, na baiskeli 50 zimesambazwa kwa wanafunzi wa vijijini ili kuwapunguzia muda wa kufika shuleni na kuongeza mahudhurio.

Msafara wa mwaka huu unaendeleza mafanikio hayo kwa kuzingatia zaidi upatikanaji wa elimu jumuishi, uhifadhi wa mazingira, na utoaji wa huduma bora za afya. Aidha, kampeni hiyo itaendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum kwa kugawa vifaa vya kusaidia kama vile viti, kwa lengo la kujenga jamii jumuishi.

Msafara huo utaanza rasmi katika viwanja vya Kijitonyama jijini Dar es Salaam na kwa mara ya kwanza zitapitia mikoa ya Pwani, Tanga, Arusha, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu hadi Mara. Katika maeneo haya, waendesha baiskeli, wadau na wanajamii watahusika moja kwa moja katika shughuli za upandaji miti, msaada wa kielimu, kambi za afya na usafi wa mazingira.

Mwanzilishi wa msafara wa Twende Butiama, Bw. Gabriel Landa, alisema: “Kilichoanza kama harakati ndogo za baiskeli sasa kimekuwa harakati ya kitaifa ya kuleta mabadiliko. Kila mwaka tunapanda miti, tunatoa elimu, na kugusa maisha ya maelfu ya Watanzania. Safari ya mwaka huu kutoka Dar es Salaam hadi Butiama ni safari ya matumaini kwa taifa letu.”

Msafara wa Twende Butiama unadhaminiwa na wadau kadhaa wakiwemo ABC Impact, ABC Bicycle, serikali za mitaa, vilabu vya baiskeli vya kitaifa na kikanda pamoja na mashirika ya maendeleo. Vyombo vya habari vinatarajiwa kuwa sehemu muhimu katika kufikisha simulizi, sauti, na nyuso za wanufaika wa msafara wa Twende Butiama.