Vyombo vya Habari vyaaswa kuelimisha umma juu ya umuhimu wa usimamizi wa mnyororo wa ugavi

0
100

Kamishna wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Dkt. Frederick Mwakibinga amewataka wamiliki na wahariri wa mitandao ya kijamii nchini kutumia vyombo vyao kueneza elimu kwa Umma kuhusu umuhimu wa kuwa na usimamizi madhubuti wa mnyororo wa Ugavi nchini.

Amesema hayo mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii ambapo amesema kupitia vyombo vya Habari, Serikali itaweza kuwafikia Watanzania wengi, kuweza kuufamu vizuri umuhimu wa usimamizi wa mnyororo wa Ugavi na kujipanga kuusimamia vizuri ili uwe na matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi.

“Tumeandaa mafunzo haya muhimu ya usimamizi wa mnyororo wa ugavi, na kupitia kwenu tungependa kuwafikia wananchi wa Tanzania, waweze kuufamu vizuri huu mnyororo na hivyo kuweza kujipanga kuusimamia vizuri ili ulete matokeo yanayotarajiwa’’ amesema Dkt. Mwakibinga.

Ameongeza kuwa shughuli za mnyororo wa ugavi zinaanzia katika upangaji wa mahitaji, ununuzi, ugomboaji na uondoshaji, upokeaji, uhifadhi, usambazaji, hadi matumizi na uondoshaji wa bidhaa, vifaa au huduma, na endapo kutakosekana kwa usimamizi madhubuti katika hatua yoyote kati ya hizi kunaweza kusababisha hasara kubwa kwa Serikali, upotevu wa rasilimali, au huduma duni kwa wananchi.

Pia, Dkt. Mwakibinga amewataka wamiliki wa mitandao ya kijamii na wananchi kwa jumla kutambua athari zinazotokana na kutokuwepo kwa usimamizi wa shughuli zote zilizopo katika mnyororo wa ugavi, kwani kwa kufanya hivyo kutaiweka serikali katika mazingira mazuri ya kutengeneza miongozo na mikakati mbalimbali ya utekelezaji ili kuimarisha usimamizi na hata kuepukana na athari hizo.

Mafunzo kuhusu usimamizi wa mnyororo wa ugavi yameendeshwa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Usimamizi wa Sera za Ununuzi wa Umma, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Send this to a friend