
Waandishi wa habari 18 wamedai kushambuliwa vikali na wanajeshi wa Uganda pamoja na maafisa wa kikosi cha kupambana na ugaidi katika eneo la Kawempe North, Kampala wakati wakiripoti uchaguzi mdogo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Reporters Without Borders (RSF), waandishi hao mmoja wao akiwa Abubaker Lubowa wa gazeti la Daily Monitor, walilazimishwa kufunika macho kwa mashati yao, kulala chini, na kupigwa kwa fimbo.
Baadhi yao wameeleza kuwa vifaa vyao vilichukuliwa na baadaye kuharibiwa, huku wengine wakisema walizuiliwa ndani ya gari la jeshi kwa masaa kadhaa bila mawasiliano huku mwandishi Raymond Tamale wa NTV akisema waliamriwa kujifanya wamelala na kukoroma, huku wakihesabu hadi 15 na kupigwa kwa kila namba.
Mkurugenzi wa RSF Kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Sadibou Marong, amelaani tukio hilo na kuitaka serikali ya Uganda kufanya uchunguzi huku akisema ukatili kutoka kwa vikosi vya usalama dhidi ya waandishi wa habari ni jambo lisilokubalika.
Msemaji wa Jeshi, Chris Magezi, amesema kuwa vurugu hizo zilitokana na kutokuelewana, na kwamba waandishi wa habari huenda walichanganywa na watu watu waliokuwa wakifanya vurugu.
Uganda inashika nafasi ya 128 kati ya 180 kwenye Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani huku mara kwa mara Waandishi wa habari wakikabiliwa na unyanyasaji wa kimwili, kuzuiwa uhuru na vikwazo vya kisheria.