Waangalizi wa Afrika Mashariki wasema uchaguzi wa Tanzania ulifuata taratibu
Waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamesema kuwa uchaguzi mkuu wa Tanzania umefanyika kwa kufuata taratibu.
Rais Mstaafu wa Burundi, Sylvestre Ntibantunganya ambaye ndiye kiongozi wa wajumbe 89 waliosambazwa Tanzania kufuatilia uchaguzi huo amesema kumekuwepo na hali ya usalama katika maeneo mbalimbali, watu wakifanya kampeni kwa uhuru kabla ya kuanza shughuli ya upigaji kura
Kiongozi huyo amesema wakiwa nchini waliweza kukutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa na waangalizi wengine.
Siku ya upigaji kura, Oktoba 28, 2020 amesema vituo vilifunguliwa kwa wakati na masuala yote ya kiufundi yalishughulikiwa vizuri na kwa wakati, na hivyo kuwaruhusu wapigakura kutimiza haki yao.
”Ujumbe wa waangalizi unatoa wito kwa vyama vya kisiasa kufuata taratibu za kisheria kuonesha kutoridhishwa kwao na matokeo. Tunatoa wito kwa vyama vya siasa kuweka mbele maslahi ya Watanzania, ikiwemo usalama na amani na kuepuka vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani,” amesema.
Waangalizi hao wamewapongeza Watanzania kwa busara walioionesha katika shughuli za wakati wa kampeni na uchaguzi kwa kuzingatia kwanza masuala ya amani na usalama.
Tayari Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) imetangaza matokeo ya urais kutoka katika majimbo zaidi ya 250, huku machache yaliyobaki yakitarajiwa kutangazwa leo.